Mwakinyo awapa kisogo mabondia wa Tanzania

Muktasari:

Mwakinyo bondia namba moja Afrika katika uzani wa super welter ndiye Mtanzania mwenye rekodi bora ya dunia hivi sasa ambako ni bondia namba 19 wa dunia kwenye uzani huo.

Dar es Salaam. Wakati mabondia wengi wa Bongo wakionyesha nia ya kutaka kuzichapa na Hassan Mwakinyo, bondia huyo amewambia muda wao bado.

Baada ya Mwakinyo kumchapa kwa Technical Knock Out (TKO) aliyekuwa bondia namba nane wa dunia, Samm Eggington ameweka rekodi ya kuwa bondia bora Afrika huku baadhi ya mabondia nchini wakitaka kuzichapa naye.

Miongoni mwa mabondia hao ni Mada Maugo, Abdallah Pazi (Dullah Mbabe) ambao wanapigania uzani wa super middle na Shaban Kaoneka ambaye ni bondia pekee aliyewahi kumchapa Mwakinyo kwa Knock Out (KO) miaka ya nyuma.

"Sijakataa kupigana na mabondia wa Tanzania, lakini kila kitu kina utaratibu wake, wakati utakapofika nitacheza na bondia yoyote yule," alisema Mwakinyo.

Alisema hivi sasa mipango yake ni kucheza mapambano ya kimataifa ikiwamo la Oktoba 26 ambalo litapigwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

"Mabondia wa Tanzania wanaotaka kupigana na mimi ni suala la muda tu, wavute subira wakati utakapofika niko tayari, sina hofu na yoyote yule, najiamini na uwezo wa kuwapiga ninao," alitamba Mwakinyo.