Rekodi nne ngumu kwa Samatta Ligi ya Mabingwa Ulaya hizi hapa

Wednesday September 18 2019

Mwanaspoti, Tanzania, Rekodi nne, Genk, ngumu kwa Samatta, Ulaya hizi hapa,

 

By Charles Abel

Dar es Salaam.Kitendo cha mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta kucheza na kufunga bao kwenye mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baina ya timu yake Genk ya Ubelgiji dhidi ya RedBull Salzburg ya Austria, kimemfanya aweke rekodi tatu tofauti

Rekodi hizo tatu zilizowekwa na Samatta kwenye mechi hiyo ambayo Genk ilichapwa mabao 6-2 ni ile ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza mashindano hayo, Mtanzania wa kwanza kufunga bao, pia Mtanzania wa kwanza kufunga bao kwenye mechi yake ya kwanza ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kabla ya hapo, Samatta aliwahi kuweka rekodi nyingine ambazo hazikuwahi kuwekwa na mchezaji mwingine yeyote wa Kitanzania kama vile, rekodi ya kuwa mchezaji ghali wa Tanzania pindi aliponunuliwa na Genk akitokea TP Mazembe, mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kufunga bao na kupachika idadi kubwa ya mabao kwenye Ligi ya Ubelgiji, Mtanzania wa kwanza kutwaa tuzo ya mchezaji Bora wa Ndani Afrika na pia Mtanzania wa Kwanza kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ubelgiji mwenye asili ya Afrika.

Hata hivyo, wakati Samatta akiweka rekodi hizo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, kuna rekodi nne za kibabe kwenye mashindano hayo ambayo anakabiliwa na mlima mrefu na anapaswa kufanya kazi ya ziada ili aweze kuzivunja.

Makala hii inakuletea orodha ya rekodi hizo nne ambazo Samatta anapaswa kupambana kwa machozi, jasho na damu aweze kuzifikia au kuzivunja.

  1. Ufungaji Bora wa muda wote
Advertisement

Kwa umri wake wa miaka 26 na aina ya timu anayochezea, ni jambo lililo wazi kwamba ni miujiza kwa Samatta kufikia au kuvunja rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kutokana na idadi kubwa ya mabao ambayo yamefungwa na mtu anayeshikilia rekodi hiyo.

Kwa sasa rekodi hiyo inashikiliwa na nyota wa Juventus, Cristiano Ronaldo ambaye amepachika jumla ya mabao 126 akifuatiwa na Lionel Messi ambaye amefumania nyavu mara 112.

Katika mabao hayo 126 ya Ronaldo, 105 ameyafunga akiwa anachezea Real Madrid, 15 kwenye kikosi cha Manchester United na sita (6) amepachika akiwa ndani ya uzi wa Juventus.

2. Mwaafrika aliyecheza idadi kubwa ya mechi

Ndio kwanza Samatta amecheza mechi moja ya mashindano hayo akiwa ni Mtanzania wa kwanza kufanya hivyo, lakini mbele yake ana rekodi nzito ya kuifikia au kuivunja ambayo ni ile ya kuwa Mchezaji wa Kiafrika aliyecheza idadi kubwa ya mechi za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa sasa rekodi hiyo inashikiliwa na Didier Drogba wa Ivory Coast ambaye yeye ameshiriki kwenye michezo 92 ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Chelsea aliyoichezea jumla ya mechi 74, Galatasaray (12) na Olympique Lyon aliyoichezea mechi sita (6)

Mwaafrika anayeshika nafasi ya pili kwa kucheza idadi kubwa ya mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya ni Samuel Eto’o ambaye amaecheza jumla ya michezo 78 katika klabu za Real Madrid, Real Mallorca, Barcelona, Inter Milan na Chelsea.

3. Mwaafrika aliyefunga idadi kubwa ya mabao

Mbwana Samatta anadaiwa jumla ya mabao 43 au zaidi ya hapo ili aifikie au aivunje rekodi inayoshikiliwa na Didier Drogba ya kuwa Mwafrika aliyefunga idadi kubwa ya mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Drogba amefunga jumla ya mabao 44 kwenye mashindano hayo akifuatiwa na Samuel Eto’o wa Cameroon ambaye amepachika mabao 30 wakati nafasi ya tatu inashikiliwa na nyota wa Liverpool, Mohamed Salah ambaye yeye amefumania nyavu mara 18.

4. Ufungaji Bora wa msimu

Hadi sasa ni Mwaafrika mmoja tu amewahi kuwa Mfungaji Bora wa msimu wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambaye ni Rais wa sasa wa Liberia, George Weah aliyefanya hivyo kwenye msimu wa 1994/1995.

Weah alipachika jumla ya mabao saba (7) katika michezo 10 akiwa na kikosi cha Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa na kabla au baada ya hapo hakuna Mwaafrika aliyeondoka na kiatu cha dhahabu cha mashindano hayo kama alivyofanya yeye.

Advertisement