Faili kesi ya Wambura larudishwa Takukuru

Muktasari:

Shauri hilo upelelezi wake haujakamilika jarada lilikuwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) walibaini kuwa kuna maeneo machache yanatakiwa kufanyiwa marekebisho hivyo jarada la kesi hilo limerudishwa Takukuru ili lifanyiwe marekebisho.

Dar es Salaam. Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa jarada la kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Michael Wambura limerudishwa  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) ili kukamilisha maeneo machache yenye upungufu.

Wambura alifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza, Februari 11, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya Sh 100milioni, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2019.

Wakili Simon alida leo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina kuwa shauri hilo upelelezi wake haujakamilika jarada lilikuwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) walibaini kuwa kuna maeneo machache yanatakiwa kufanyiwa marekebisho hivyo jarada la kesi hilo limerudishwa Takukuru ili lifanyiwe marekebisho.

"Upelelezi bado na shauri hili lilikuja kwa ajili ya kutajwa hivyo naiomba mahakama yako ihairishe shauri hili, alidai Simon.

Hakimu Mhina alisema shauri hilo litakapokuja mahakamani hapo wahakikishe upande wa mashtaka wanaeleza wamefikia kwenye hatua gani. Shauri hilo limeahirishwa hadi Oktoba 2, 2019 litakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Katika mashtaka hayo 17; shtaka moja ni la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Katika shtaka la kwanza la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2004, sehemu isiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Siku hiyo, Wambura kwa nia ya kutapeli alitengeneza barua ya  kughushi ambayo haina kumbu kumbu namba akionyesha  imeandikwa na E Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa  kampuni ya Jeck system anadai kurejeshewa malipo ya mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka la kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, mshtakiwa  alitoa barua iliyokuwa haina kumbu kumbu namba  ya Julai 6, 2004, akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck System Ltd, akionyesha kuwa anadai mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo, kuanzia shtaka la tatu hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia kiasi cha zaidi Sh 95 milioni, kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbali mbali na riba kutoka kwa kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua kuwa siyo kweli.

Pia katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadiawa kutenda kosa hilo, Juni 17, 2015 huko katika ofisi za TFF, ambapo kwa njia ya udanganyifu, mshtakiwa alijipayia Sh 10milioni kutoka TFF kwa kuonesha kuwa ni malipo ya USD 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ha Jeck jambo ambalo siyo kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadai, kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014, makao makuu ya Shirikisho hilo,  alijipatia Sh 25milioni  kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Pia, shtaka jingine utakatishaji fedha haramu, Mshtakiwa anadaiwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21 2015, alijipatia Sh 75,947,924 kutoka TFF wakati akijua fedha hizo siyo halali na zimetokana na shtaka la kughushi.