Yanga, Azam ushindi kokote kwa Zesco, Triangle United

Muktasari:

Uteuzi wa mbinu nzuri kwenye  mechi ya marudiano kwa walimu wa makocha wa timu hizo, Mwinyi Zahera wa Yanga na Etienne Ndayiragije wa Azam ni jambo linaloweza kuzibeba Yanga na Azam FC ugenini licha ya matokeo yasiyoridhisha.

Dar es Salaam. MASHABIKI wa soka wamepatwa na ganzi kutokana na matokeo ya mechi za raundi ya kwanza ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kwa timu za Azam na Yanga na hata Malindi Zanzibar, yamekwenda kinyume na kile kilichotarajiwa na wapenzi na mashabiki wengi wa soka.
Timu hizo zilishindwa kutumia vyema viwanja vya nyumbani na kujikuta kila moja ikishindwa kuvuna ushindi ambao ungeweza kuwa kuwaweka katika nafasi nzuri kwa mechi zao za marudiano wiki mbili zijazo.
Yanga inayoshiriki Ligi ya Mabingwa ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Zesco ya Zambia, Jumamosi wakati siku inayofuata Azam ilipoteza mbele ya Triangle United ya Zimbabwe kwa bao 1-0 na Malindi ilichapwa mabao 4-1 na Al Masry ya Misry katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Ni wazi ni vigumu kwa Malindi kupindua meza ugenini na kuwatua nje Al Masry lakini upo uwezekano wa Yanga na Azam kufanya hivyo kwenye mechi za marudiano ugenini.
Tathmini ya gazeti hili imebaini sababu nne ambazo huenda zikawa chachu kwa Yanga na Azam kwenda kutikisa ugenini na kupata ushindi kinyume na matarajio ya wengi na kama nyota wa timu hizo, yaani Obery Chirwa na wenzake wa Azam sambamba na kina Juma Balimba na Patrick Sibomana wa Yanga wakiamua kukomaa kibabe.
Uteuzi wa mbinu nzuri kwenye  mechi ya marudiano kwa walimu wa makocha wa timu hizo, Mwinyi Zahera wa Yanga na Etienne Ndayiragije wa Azam ni jambo linaloweza kuzibeba Yanga na Azam FC ugenini licha ya matokeo yasiyoridhisha.
Azam kwenye mechi ya kwanza ilikosa mpango mbadala kwenye safu ya ushambuliaji ambapo kwa muda mrefu ililazimisha kupenya kwa kupitia katikati ambayo ilishindwa kufanya kazi kutokana na ubora wa wapinzani wao ambao walishtukia na kujipanga kuwadhibiti.
Kwenye mechi ya marudiano, iko haja ya Azam kubadilika kuongezea na mbinu ya kutumia mipira ya krosi ambayo ilionekana kuwatesa Triangle United katika dakika za mwisho za mechi ya kwanza lakini.
Ni kama ilivyo kwa Yanga ambayo inahitajika kushambulia zaidi kutokea pembeni kwa kuanza na mawinga wawili asilia badala ya kujaza idadi kubwa ya viungo ambao kiasili ni wakabaji, jambo linaloweza kupunguza ufanisi wa kutengeneza nafasi na mabao.
Hata hivyo, jambo la pili linaloweza kuzibeba Yanga na Azam ni upangaji mzuri wa kikosi, pia umakini wa kufanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi.
Ni moja ya eneo ambalo limeziangusha katika mechi za kwanza nyumbani kwani baadhi ya wachezaji ambao walianza hawakuonyesha kutoa mchango mkubwa huku mabadiliko yaliyofanyika yakiziathiri pia kwa namna moja hasa kutokana na kuingiza wachezaji ambao hawakwenda kuongeza kitu uwanjani na kuwatoa wale ambao walikuwa na mchango mkubwa.
Mfano wa hilo ni kitendo cha Azam kumtoa Richard Djodi aliyekuwa msumbufu kwa mabeki wa Triangle na kumuingiza Shaaban Idd ambaye hata hivyo alionekana kushindwa kutimiza majukumu aliyopewa na kujikuta akitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Idd Kipagwile.
Kwa Yanga, walishindwa kunufaika na mabadiliko ya kumtoa Sadney Urikhobi na kumuingiza Maybin Kalengo ambaye hakuwa na msaada kwenye safu yao ya ushambuliaji na kumuacha nje, Juma Balinya ambaye mbali na uwezo wa kufunga ana sifa ya ziada ya uwezo mkubwa wa kufunga kutokana na mipira iliyokufa jambo ambalo pengine lingeiokoa Yanga.
Wawakilishi hao wa Tanzania pia wanapaswa kuhakikisha wanatangulia kufunga bao ugenini, ili kuwaongezea mzigo na kuwaweka wenyeji wao kwenye presha kubwa na kuwalazimisha wabadili mbinu za mechi hizo za marudiano.

USHINDI KOKOTE
Jambo lingine ambalo likawa chachu kwa Yanga na Azam kupata ushindi ugenini ni rekodi ya kushinda baadhi ya mechi za ugenini kwenye mechi za kimataifa ambazo iliwahi kucheza hapo nyuma.
Rekodi hizo za ushindi huenda zikazi weka timu hizo kwenye hali nzuri kisaikolojia kuweza kupambana na kusaka ushindi kwenye mechi zao.
Ni raundi iliyopita tu, Yanga iliibuka na ushindi ugenini wa bao 1-0 dhidi ya Township Rollers baada ya kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani.
Kana kwamba haitoshi, mwaka 2017 Yanga ilishawahi kupata ushindi ugenini dhidi ya Ngaya Club ya Comoro kwa mabao 5-1 lakini pia iliwahi kuichapa Cercle Joachim ya hukohuko kwa bao 1-0 mwaka 2016.
Hata Azam FC imewahi kufanya hivyo mara kadhaa pindi iliposhiriki mashindano ya kimataifa.
Mwaka 2013 ilichapa El Nasir ya Sudan Kaskazini kwa mabao 5-0 ugenini huko Juba na baadaye ikaifunga Barrack Young Controllers II ya Liberia kwa mabao 2-1 ugenini.
Pia mwaka 2016, Azam iliichapa timu ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa mabao 3-0 ugenini kwenye raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.

WASIKIE WADAU SASA
Mchambuzi wa soka, Mwailimu Alex Kashasha na beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa walisema Yanga na Azam zina nafasi ya kufanya vizuri ugenini ikiwa watafanyia kazi mapungufu ya mechi zilizopita.
“Kinac hotakiwa kwa sasa ni walimu kutafakari kwa kina nini kiliwaangusha kwenye mechi za juzi na  baada ya hapo watapata mbinu za kuweza kuzitumia kwenye mechi za marudiano.
Yanga walia nguswa na kukosa idadi kubwa ya wachezaji kwenye eneo la timu pinzani pindi walipokuwa wanashambuliwa hivyo wakifanikiwa kurekebisha hilo, wana nafasi ya kushinda ugenini.
Azam waliumizwa na kosa la kutaka kushambulia kwa mbinu ileile ya kupiga pasi fupi za kupenyeza kuingia langoni mwa timu pinzani hivyo wanapaswa kuwa na mbinu mbadala ugenini,” alisema Mwalimu Kashasha.
Naye Pawasa alisema kuwa Azam na Yanga zikiongeza umakini kwa wachezaji zitapata ushindi.
“Nafasi wanayo lakini ni ngumu ukizingatia mazingira ya soka la Afrika. Kikubwa nilichokiona ni wachezaji kukosa umakini na kucheza huku wakihisi watapa ushindi kirahisi kwa sababu wanacheza nyumbani.
Wanakwenda ugenini ambako wanatakiwa wacheze kwa utulivu na nidhamu ya hali ya juu ambayo ndio itakuwa silaha ya mafanikio kwao vinginevyo watakuwa kwenye wakati mgumu,” alisema Pawasa.