Yanga yaifuata Zesco mapema hatma ya Molinga kwa CAF

Muktasari:

Mabosi wa Yanga akili zao zote kwa sasa ni kuhakikisha wanapindua meza mjini Ndola na kuipeleka timu Zambia mapema ikajifue kwa siku tano kabla ya mchezo wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ametaka timu iende mapema Zambia kwa siku tano zaidi na tayari mabosi wake kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Rodgers Gumbo amethibitisha kikosi hakitakuwepo nchini wiki ijayo.

Mabosi wa Yanga akili zao zote kwa sasa ni kuhakikisha wanapindua meza mjini Ndola na kuipeleka timu Zambia mapema ikajifue kwa siku tano kabla ya mchezo wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Ni kweli kocha ametuomba hilo na litatekelezeka tunachotaka ni ushindi hakuna lingine tutafanya kama tulivyofanya Botswana, tunataka kuzoea hali ya kule mapema na kuna wenzetu wawili watatangulia,” alisema Gumbo.
“Uongozi hatujakata tamaa tunaimani Zesco inapigika kwao, bado tutatoa ushirikiano kwa makocha na wachezaji kuhakikisha tunafikia malengo ya kutinga hatua ya makundi hiyo ni vita tutakayopigana na Zesco mchana kweupe,” aliongeza.

ZAHERA AFICHUA
Kocha Zahera alifichua kilichoiponza Yanga timu yake kutoifunga Zesco ni safu ya ushambuliaji na katika maandalizi amezingatia katika eneo hilo.
Zahera alisema kutotumia nafasi ndiyo kuliwaangusha, lakini kwa kazi ambayo itafanyika Zesco haitakuwa na mchezo mwepesi wakiwa kwao mjini Ndola, Zambia.
“Tuliangushwa na ufanisi mdogo wa washambuliaji, ingekuwa timu haitengenezi nafasi ningesema hilo ni tatizo letu, lakini shida ni kumalizia, angalia nafasi kama aliyopata Patrick (Sibomana) akajigonga tukashindwa kufunga,” alisema Zahera.
Kuhusu Juma Balinya ambaye hakucheza mchezo huo, lichja ya kuivusha Yanga katika raundi hiyo kwa bao lake la mjini Gaborone, Botswana dhidi ya Township Rollers, Zahera alisema straika huyo raia wa Uganda aliongezeka uzito kwa kilo nne zaidi, hivyo kushindwa kuendana na kazi anazotaka azifanye ndani ya uwanja.
“Tulishaanza kazi ya kumpunguza uzito tangu tukiwa Mwanza akapungua kilo mbili na kazi hiyo itamalizika katika muda uliosalia ili tuangalie kama tunaweza kumtumia.”

Katika hatua nyingine sakata la David Molinga ‘Falcao’ akimkurupusha kigogo mmoja wa klabu hiyo kukimbilia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuseti mambo.
Tuanze na ishu ya Molinga kwanza. Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo amefichua uongozi wao uko katika mapambano ya kukamilisha usajili wa straika wao aliyeanza kutupia kwenye mechi za kirafiki, Molinga na beki Mustapha Seleman ili wakiifuata Zesco wawe kamili gado.
Gumbo alisema wamefichuliwa kuna uwezekano wa timu yao kuwapata wachezaji hao na endapo itashindikana kupata suluhu hiyo hapa nchini watamsafirisha bosi mmoja kwenda Cairo, Misri yalipo Makao Makuu ya CAF.
“Tumepata hizo taarifa sasa na kweli tunahitaji huduma ya Molinga na Mustapha kazi hiyo ndiyo tunapambana nayo sasa  na kama itashindikana kukamilika tukiwa hapa tunamtuma mtu kwenda Caf kama ni faini tutalipa ili wapatikane,” alisisitiza Gumbo.