Man City, Chelsea, Liverpool, Barca, Real huu hapa mtoko wote wa Ligi ya Mabingwa Ulaya

Tuesday September 17 2019

Man City, Chelsea, Liverpool, Barca, Real huu hapa mtoko wote, Mwanaspoti, Tanzania, Ligi ya Mabingwa Ulaya

 

Madrid, Hispania. Hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa 2019/20 inaanza rasmi leo Jumanne kwa mechi kadhaa kabla ya mchakamchaka mwingine kuendelea kesho Jumatano.
Liverpool mabingwa wa msimu uliopita, walipowachapa Waingereza wenzao Tottenham kwenye mchezo wa fainali, watakuwa na kazi moja ya kutaka kutetea ubingwa huo, ambapo itakuwa mara yao ya saba kama watafanikiwa kulibeba taji hilo.
Kikosi cha Pep Guardiola, Manchester City kinatarajiwa kuja kivingine baada ya kushindwa kufika nusu fainali tangu msimu wa 2015/16, lakini mikikimikiki hiyo inashirikisha wababe watupu wakiwamo Barcelona, Real Madrid, Bayern Munich, Paris Saint-Germain na Juventus, ambao wote wamepania kufanya kweli msimu huu.
Wakati ukisubiri kwa hamu mechi hizo, hivi hapa vitu ambavyo ungepaswa kuvifahamu kuhusiana na michuano hiyo, namna inavyonoga!

Msimu wa 50 kwa Real Madrid
Ligi ya Mabingwa ya mwaka huu, itakuwa maalumu kwa Real Madrid, ambapo utakuwa msimu wake wa 50 kushiriki michuano hiyo na ndio maana imeweka historia tamu kwa kubeba ubingwa mara nyingi.
Miamba hiyo ya Hispania inashikilia rekodi ya kubeba ubingwa wa taji hilo mara 13, ambapo huko nyuma iliwahi kubeba mara tano mfululizo kati ya 1955 na 1960, kabla ya miaka ya karibuni kulibeba misimu mitatu mfululizo 2015/16, 2016/17 na 2017/18 wakiwa chini ya Kocha Zinedine Zidane.  Safari hii imepangwa Kundi A sambamba na PSG, Club Brugge na Galatasaray.

Zidane hajawahi kufungwa
Kocha wa Madrid, Zinedine Zidane mwenyewe atahitaji kuweka rekodi yake kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Hakuna kocha aliyebeba ubingwa huo wa Ulaya mara nne, hivyo Mfaransa huyo aliyenyakua mara tatu sawa na ilivyo kwa Bob Paisley na Carlo Ancelotti anataka kubeba kwa mara ya nne. Lakini, kitu kitamu, Zidane anashikilia rekodi ya kwamba hajawahi kutupwa nje ya michuano hiyo tangu awe kocha wa Real Madrid. Msimu uliopita, wakati Real Madrid iliposukumwa nje na Ajax kwenye hatua ya 16 bora, kocha wa Los Blancos alikuwa Santiago Solari, aliyerithi timu kutoka kwa Julen Lopetegui, baada ya Zidane kuondoka mwishoni mwa msimu.

Messi hana maajabu kwa Inter
Staa wa Barcelona, Lionel Messi amefunga mabao 112 katika misimu yake 15 aliyocheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kushinda ubingwa huo mara nne. Hakuna timu inayopenda kukabiliana na Messi, hasa msimu huu wakati Barca itakapocheza na Borussia Dortmund, Inter Milan na Slavia Prague kwenye Kundi F. Lakini, unaambiwa hivi, ujanja wake wote Messi, huwa hawafungi Inter.
Wakali hao wa Serie A ni moja kati ya timu tano ambazo Messi hajazifunga kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakiwamo Atletico Madrid aliokutana nao mara nne, Rubin Kazan mara mbili, Benfica na Udinese mara moja. Messi amecheza dhidi ya Inter mara tatu kwenye michuano hiyo ya Ulaya na hajafunga, huku timu yake ikipata ushindi mara moja tu.  Inasubiriwa kuona kama Oktoba 2 ataifunga Inter huko Nou Camp au ile ya marudiano San Siro, Desemba 10.

Nou Camp pagumu usipime
Uwanja wa nyumbani wa Barcelona, Nou Camp ni mahali pagumu sana kwa timu pinzani zinapokwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya uwanjani hapo. Nou Camp kwa sasa inashikilia rekodi ya kuchezwa mechi 32 bila ya timu ya ugenini kupata ushindi, ambapo mara ya mwisho Barcelona kupoteza kwenye uwanja huo, ilikuwa msimu wa 2012/13 ilipochapwa 3-0 na Bayern Munich, zaidi ya miaka sita iliyopita.
 Timu 24 tofauti zimekwenda kucheza uwanjani hapo tangu wakati huo na hakuna iliyopata ushindi. Rekodi ya mechi nyingi zaidi za nyumbani bila ya kupoteza inashikiliwa na Bayern Munich, ambapo ilidumu kwa mechi 43 mfululizo bila ya kupoteza kwenye michuano hiyo ya Ulaya kuanzia 1969 hadi 1991.

Benzema afukuzia rekodi ya Giggs
Messi au Ronaldo ni majina yanayoboa kutokana na kutamba kwenye soka kwa muda mrefu. Karibu miaka 10 wamekuwa wakigawana tu Ballon d’Or, huku wakitamba pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Msimu huu wanaweza kufanya kitu kingine, lakini Karim Benzema anaweza kuingia katikati yao. Wakali hao watatu, yeyote atakayefunga, basi watapiku rekodi wanayoshikilia kwa pamoja na staa wa zamani wa Real Madrid, Raul ya kufunga mabao kwenye misimu 14 mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akifunga ndani ya msimu huu, basi Benzema atakuwa amejisogeza karibu kabisa katika kuifikia rekodi inayoshikiliwa na gwiji wa Manchester United, winga Ryan Giggs, aliyefunga kwenye misimu 16 tofauti katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ajax imeanzia mbali
Miamba ya soka ya Uholanzi, Ajax iliwaduwaza mashabiki wa Ulaya baada ya kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, lakini ilishindwa kufuzu moja kwa moja hatua ya makundi ya michuano hiyo msimu huu kutokana na nafasi ya ligi ya Eredivisie kwenye viwango vya UEFA.
Kutokana na hilo, imeshacheza mechi nne kwenye michuano hiyo msimu huu, ambapo ilianzia kwenye raundi ya tatu ya kufuzu, ikiifunga PAOK na APOEL kabla ya kuingia kwenye hatua ya makundi. Itaanza kampeni yake rasmi kwenye hatua ya makundi kwa kucheza na Lille ya Ufaransa.

Luis Suarez wa ugenini ni majanga
Luis Suarez anapenda kuichezea Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Si tu amebeba ubingwa, bali amekuwa na rekodi nzuri ya kufunga, akitikisa nyavu mara 20 katika mechi 48 alizoitumikia timu hiyo ya Nou Camp. Lakini fowadi huyo kwa sasa anashikilia rekodi mbaya asiyoitaka, kushindwa kufunga kwenye mechi za ugenini kwa muda mrefu sana.
Mara ya mwisho, Suarez kufunga ugenini kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa msimu wa 2015/16 kwenye sare ya 1-1 dhidi ya AS Roma huko Italia. Baada ya hapo, straika huyo wa zamani wa Liverpool amecheza zaidi ya dakika 1,691 bila ya kufunga bao ugenini kwenye michuano hiyo ya Ulaya.

Atalanta mechi za nyumbani ni Milan
Atalanta wapya hawa kwenye michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu huu na wengi wanaamini wanaweza kupenya na kuvuka kwenye hatua ya makundi.
Misimu miwili iliyopita walitamba kwenye Europa League, lakini baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye Serie A msimu uliopita mbele ya AS Roma, AC Milan na Inter wamepata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Lakini, uwanja wao wa nyumbani, uwezo wake ni kuingiza watazamaji 21,300, hivyo hauendani na taratibu za Uefa na kuwafanya wababe hao kuhamishia mechi zao kwenye Uwanja wa San Siro.
 Milan hawatatumia uwanja huo kwa michuano ya Ulaya msimu huu, kwa sababu hawajafuzu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League pia wamepigwa marufuku baada ya kukiuka sheria ya usawa wa mapato na matumizi.

Advertisement