Bandari yapania kunyorosha Mwarabu kwao

Tuesday September 17 2019

Bandari, Mwanaspoti, kunyorosha, Mwarabu kwao, Kenya, Tanzania, CAF, Tunisia

 

LICHA ya kupata ushindi mzuri wa mabao 2-0 dhidi ya Mtunisia US Ben Guerdane juzi kati uwanjani Kasarani kwenye mchujo wa kufuzu hatua ya makundi katika dimba la CAF Confederation, kocha wa Bandari FC Bernard Mwalala yupo rada kinoma.
Kwa ushindi huo, Bandari sasa wanahitaji sare ya aina yoyote watakaporudiana  na Waarabu hao ugenini ili kutinga hatua ya makundi  ya dimba hilo.
Mwalala tayari kaanza mikakati ya kuhakikisha ndoto yao inatimia, kikubwa zaidi akiwa anawazia mbinu ya namna watakavyokaza kule Tunis kuhakikisha Mwarabu hayakomboi mabao hayo.
“Tumekuwa tukijitahidi sana mazoezini kuboresha safu yetu ya mashambulizi na nashukuru tulipata magoli mawili ukizingatia ni nafasi chache sana tuliweza kutengeneza. Kule tunakwenda kudifendi na kama wakizubaa tuwawahi bao la ugenini. Kiufundi Watunisia wapo vizuri na wanajua kushambulia hivyo lazima tuwakazie, tumeajiandaa kudefendi kinoma,” Mwalala kasema.

Walivyowafumua Waarabu
Kwenye mechi ya Jumamosi ambayo Mwalala awali alionyesha kupaniki kidogo akiwataja Waraabu kuwa bora kuwaliko wao, Bandari waliishia kuonyesha kiwango.
Mechi ilianza kwa kasi lakini kwa mara nyingine tena, Bandari ambao wamekuwa wakitatizika sana  kufunga bao ndani ya dakika 90  katika mechi zao tano za mwisho kabla ya Mwarabu, walionyesha dalili ya kumaliza ngoma hiyo sare.
Hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza, Bandari walikuwa wamendikisha shoti moja pekee langoni likitoka kwake Abdallah Hassan baada ya kuzalishiwa krosi tamu na Cliff Kasuti dakika ya 20. Hata hivyo mkiki huyo ulidhibitiwa vyema na kipa wa upinzani.
Katika kipindi cha pili Mwalala alifanya mabadiliko yaliyolipa kwa kuwaleta mawing’a wawili wenye kasi. Shaban Kenga alichukua mahala pake Kasuti naye Benjamin Mosha akiingia kwa nafasi ya Danson Namasaka.
Mabadiliko hayo ndiyo yaliyochangia kupatika kwa mabao mawili ndani ya dakika tano. Dakika ya 73, fowadi Mcongo Yema Mwana aliunganisha vyema mpira wa kona kutoka kwa Abdallah Hassan hadi wavuni. Dakika tano baadaye ikawa zamu yake Abdallah akifunga goli la kichwa baada ya kumaliza krosi ya mpira wa kona kutoka kwake William Wadri.

Difensi imekaa vizuri
Safu ya ulinzi ya Bandari ikiongozwa na Felly Mulumba, Brian Otien, Fred Nkata na Nicholas Meja ilielendelea kuonyesha ubora wake huku naye kipa Miachel Wanyika akionyesha karithi vyema glavu zake Farouk Shikalo aliyeinua zake Bongo.
Ikiwa ni mara ya pili ya Bandari kushiriki dimba hili, tayari safari hii wamefika mbali ikilinganishwa na matokeo yao ya 2016 na walibanduliwa kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya mchujo.

Advertisement