Judo watumia Sh 30Milioni kambi wiki mbili Japan

Muktasari:

Judo ni miongoni mwa michezo inayopewa nafasi ya kufuzu kushiriki Olimpiki ya 2020 nchini Japan, ingawa sasa watasubiri kuona kama watapewa nafasi ya upendeleo na Shirikisho la Kimataifa la mchezo huo (IJF) baada ya wachezaji watano wa Tanzania kukosa vigezo kwenye mashindano ya dunia.

Dar es Salaam.Chama cha Judo Tanzania (Jata) kimesema kambi ya wiki mbili ya wachezaji wa timu ya Taifa nchini Japan imegharimu Sh 30 Milioni.

Wachezaji wawili wa Tanzania bara ni miongoni mwa nyota walioweka kambi jijini Tokyo yalipo makao makuu ya judo ya dunia kwenye eneo la Kodocan kwa mafunzo maalumu ya mchezo huo siku chache baada ya kumalizika mashindano ya dunia.

Wachezaji hao ni Andrew Thomas na Thomas Mwenda ambao watarejea nchini kesho Jumanne baada ya jana Jumapili kumaliza mafunzo hayo ya wiki mbili.

"Ni mafunzo ambayo yametoa mwanga kwa wachezaji wetu kutokana na ukubwa na ubora wake, tunatarajia watakapowasili nchini nao wawafundishe wenzao," amesema rais wa Judo Tanzania, Hamis Mgowe.

Alisema kambi hiyo imewapa uzoefu kwani wameweza kukutana na mabingwa mbalimbali wa judo wa dunia sanjari na kufundishwa na makocha wenye kiwango bora katika mchezo huo.

"Ni mafunzo ambayo yamegharimu zaidi ya Sh 30 Milioni kwa wachezaji wawili wa Tanzania bara ambao wamefadhiliwa na nchi ya Japan, kama chama tusingeweza kuwapeleka bila ufadhili huu," alisema.

Thomas na Mwenda ni miongoni mwa nyota watano wa timu ya Taifa walioiwakilisha nchi kwenye mashindano ya dunia yaliyomalizika Agosti 30 kabla ya kuanza kambi ya dunia Septemba Mosi.

Wengine ni Abdulrabi Alawi, Mansab Alawi na Ali Khamis Hussein kutoka Zanzibar ambao kwa mujibu wa Mgowe, wao watasalia nchini Japan kwa mwezi mmoja zaidi katika mafunzo wakiwa na kocha Mzanzibar mwenye asili ya Japan, Shimahoka.