Jezi za Zesco kila kona Dar

Muktasari:

Yanga inacheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika raundi ya kwanza na Zesco United ya Zambia huku jezi za wageni hao zikionekana kuuzwa jijini Dar es Salaam.

JEZI za wapinzani wa Yanga, Klabu ya Zesco United zimejaa jijini Dar es Salaam kutokana na baadhi ya mashabiki wa Simba kudai kuwa watawaunga mkono, huenda biashara hiyo ikatembea sana.
Zesco inacheza na Yanga mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mechi ya raundi ya kwanza leo Jumamosi huku watani wao wa jadi kupitia msemaji wao, Haji Manara kuweka wazi kuwaunga mkono Wazambia.
Kauli hiyo imepokelewa na sehemu kubwa ya mashabiki wa Simba ambao baadhi yao waliahidi kujitokeza kwa wingi uwanjani kwa ajili ya kuishangilia timu hiyo ya Zesco.
Jezi hizo zimeonekana zaidi Uwanja wa Taifa ambako mchezo huo utapigwa jioni ya leo saa 10:00.
Kwa sasa Zesco inafundishwa na Mzambia George Lwandamina ambaye aliifundisha Yanga miaka ya nyuma, lakini ina kiungo Thabani Kamusoko aliyemaliza mkataba wake na Yanga msimu uliopita.
Ikumbukwe pia, matukio kama hayo ni ya kawaida kwa timu hizo mbili zenye ushindani wa juu na zaidi kwenye rangi ambapo Yanga ni njano na kijani na Simba ni nyekundu na nyeupe.