Ronaldinho aamua kurudi upya uwanjani kucheza soka Colombia

Thursday September 12 2019

Ronaldinho, Mwanaspoti, Tanzania, aamua kurudi, upya uwanjani, kucheza soka, Colombia

 

RIO DE JANEIRO, BRAZIL. FUNDI wa mpira Mbrazili, Ronaldinho ameamua kuibuka kutoka mtaani na kurudi kwenye soka baada ya kutangaza kustaafu miezi kadhaa iliyopita.
Staa huyo wa zamani wa Barcelona na AC Milan mwenye umri wa miaka 39 atakwenda kuichezea Klabu ya Independiente Santa Fe ya Colombia katika mchezo utakaopigwa Oktoba 17.
Bado haifahamiki kama huo utakuwa mwanzo rasmi wa kurudi kwenye soka kwa Mbrazili huyo aliyechezea mechi 97 kwenye Timu Taifa ya Brazil, lakini pia wapinzani atakaomenyana nao bado hawajafahamika.
Santa Fe ni moja kati ya klabu yenye mafanikio makubwa kwenye soka la Colombia, ikishinda mataji 17 ya ligi. Haijawahi kushuka daraja kutoka kwenye Categoria Primera A, ligi ya daraja la juu zaidi huko Colombia.
Kiingilio kwenye mechi hiyo kimetajwa kwamba, tiketi ya bei ya juu zaidi itakuwa Pauni 30 pamoja na VAT. Jambo hilo linafanyika kuwapa mashabiki utamu wa kumshuhudia tena uwanjani fundi wa mpira akifanya mambo yake. Tiketi ya bei rahisi inatajwa kuwa ni Pauni 7.
Kumekuwa na imani kwamba huenda Ronaldinho akatumia mechi hiyo kama mwanzo wake wa kurudi kwenye mchezo wa soka na kucheza kwa miaka mingine kadhaa kabla ya kung'atuka moja kwa moja.
Huko Brazil, Ronaldinho amedaiwa kukabiliwa na matatizo ya kujenga bwawa la samaki kwenye eneo lisiloruhusiwa, huku kukwama kwake kulipa kodi kumemsababishia matatizo makubwa na mamlaka za kodi huko Brazil.

Advertisement