Zahera akomalia ufungaji Yanga ikijianda kuivaa Toto African

Muktasari:

Yanga kesho itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Toto African kwenye Uwanja wa Nyamagana, viingilio Sh 3000, mzunguko Sh 5000.

Mwanza. Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ameweka nguvu zake katika safu ya ushambuliaji kuhakikisha inatumia vizuri nafasi wanazopata kufunga mabao.

Kocha Zahera katika mazoezi ya jioni kwenye Uwanja wa Nyamagana alitumia muda mwingi wa mazoezi hayo kuwaelekeza washambuliaji wake namna ya kufunga.

Zahera alianza kuwapa wachezaji wake mbinu mbalimbali za namna ya kufunga, akionekana kuwa mkali pale wachezaji wake walipoonekana kukosa umakini.

Zahera alionekana kuwasisitiza zaidi wachezaji wake kufunga tofauti na maeneo mengine msisitizo huo kwenye mazoezi ya leo.

Mazoezi yalikuwa ya mwisho kwa Yanga kabla ya kuwavaa Toto Africans kesho ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika dhidi ya Zesco United utakaofanyika September 14 Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mashabiki wafurika mazoezini

Mashabiki wa Yanga wamejitokeza kwa wingi kushuhudia mazoezi ya timu yao yaliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana.

Mashabiki wa Yanga walifika mapema uwanjani hapo kusubiri timu yao ambayo imefika mazoezini saa kumi jioni ikiongozwa na kocha Zahera.

Shabiki atolewa mzobemzobe mazoezini

Shabiki mmoja ambaye hakufahamika jina lake amejikuta taabani leo kwa kuondoshwa 'mzobemzobe' na kutolewa nje ya uwanja kwa madai ya kuwatukana wachezaji wa Yanga.

Tukio hilo limetokea leo Septemba 9 wakati Yanga ikiendelea na mazoezi yake katika uwanja wa Nyamagana kujiandaa na mchezo wake wa kirafiki dhidi ya Toto Africans na mechi ya kimataifa ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Shabiki huyo alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya wenzake kutofurahia kauli zake kwa kuwatukana wachezaji, jambo ambalo limewachukiza na kuamua kumtoa nduki jukwaani na kumtaka aondoke kabisa maeneo hayo.

Hata hivyo shabiki huyo alionekana kutii amri na kusindikizwa na makomandoo moja kwa moja hadi nje ya geti na kuwaacha wenzake wakiendelea kushuhudia mazoezi.