Salamba aanza kufurahia maisha ya soka ndani Kuwait

Muktasari:

Hapa tunamzungumzia Adam Paul Salamba aliyetimkia Al-Jahra SC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Kuwait yaani Kuwait Division One ambayo wiki iliyopita alikuwa na timu hiyo jijini Istanbul, Uturuki kwenye kambi wakijiandaa na msimu mpya wa ligi inayoanza Septemba 18.

NJE ya Bongo imepiga kambi Kuwait kumwangazia nyota wa zamani wa Stand United, Lipuli FC pamoja na mabingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita, Simba SC wanaosaka taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuanza vyema msimu kwa kuifunga JKT Tanzania mabao 3-1.
Hapa tunamzungumzia Adam Paul Salamba aliyetimkia Al-Jahra SC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Kuwait yaani Kuwait Division One ambayo wiki iliyopita alikuwa na timu hiyo jijini Istanbul, Uturuki kwenye kambi wakijiandaa na msimu mpya wa ligi inayoanza Septemba 18.

ALIKOANZIA
Chipikuzi huyo alizaliwa miaka 19 iliyopita na maisha yake ya soka alianza kukipiga pale Bulyanhulu FC ya Shinyanga kabla ya kwenda kwenye majaribio kwa wapiga debe ‘Stand United’ wanaohaha kwa sasa kurudi Ligi Kuu baada ya kushuka msimu uliopita pamoja na African Lyon iliyoburuza mkia ikiwa na pointi 23.
Alipotua Stand, alikutana na Kocha Patrick Lewing ambaye alimchagua na kumpeleka kikosi cha vijana, na baadaye kupandishwa timu ya wakubwa aliyodumu nayo kwa msimu mmoja na kutimkia Lpuli FC.
Baada ya kuupiga mwingi akiwa na chama hilo ndipo mabosi wa Simba wakavutiwa naye ili atue Msimbazi japo mambo hayakumnyokea kivile.
Msimu uliopita mabosi wa Simba wakafumba macho kwa Salamba aliyetesa nyavu za wapinzani katika msimu wa 2017/18 kwa kufumania nyavu kila mara ili kunasa saini yake, hivyo mapema mwaka jana wakatumia Sh30 milioni pamoja na gari aina ya Toyota Crown ambalo siku chache lilipatwa ajali eneo la Vigwaza mkoani Pwani.

HAKATI TAMAA
Alipotua Simba, wengi walihoji ujio wake hasa kwa kuangalia ushindani wa namba jinsi ulivyokuwa mgumu kwa vijana wa Kocha Patrick Aussems, tena wakiwa wanashiriki mashindano ya kimataifa (Ligi ya Mabingwa Afrika).
Katika kikosi cha Simba kilichokuwa kimetoka kumsajili Meddie Kagere kutoka Gor Mahia ambaye alikuwa amemaliza mkataba na matajiri hao wa‘Kogalo’, pia ndani ya Simba alikuwapo John Bocco, Emmanuel Okwi - mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2017/18 akiwa na mabao 19.
Kuwepo kwao kulimfanya Salamba pamoja na Marcel Kaheza aliyerudishwa Majimaji FC mambo yao kwenda hovyo na baadaye akatimkia Ligi Kuu Kenya kukipiga kwenye kikosi cha AFC Leopards, huku Salamba akipewa nafasi kwa kuvizia.
Kumalizika kwa msimu uliopita kulimpa nafasi ya kwenda kujaribu maisha kwa kufanya mazunguzo na uongozi wa Klabu ya TS Sporting ya Afrika Kusini, lakini mambo yakaenda kombo ikabidi arudi nyumbani na kwenda Namungo FC alikopelekwa kwa mkopo.

AL JAHRA YAMNASA
Siku chache tu baada ya kuwasili Namungo FC akavutiwa waya na mabosi wa Al-Jahra SC ambao walimpa ofa nono na kumuomba aende Uturuki ilipoweka timu kambi ili wakamalizane naye kama atakubaliana nao.
Salamba amesaini mkataba wa miaka mitano akivuta Dola 5,000 (Sh11,487,000) za kukubali kusaini, mshahara wake ukiwa Dola 4,000 (Sh9,189,590) kwa mwezi pamoja na asilimia 25 ya nyongeza kila mwaka kutokana na kiwango chake (ambazo ni zaidi ya Sh300,000), huku Simba ikivuta Dola 45,000 zaidi ya Sh100 milioni.
Pia atapewa Dola 1,000 (Sh2,293,690) kwa kila goli atakalofunga na Dola 12,000 (Sh27,524,300) kama atafikisha mabao 20 mwishoni mwa msimu. Kwa kifupi pesa kwake ni nje-nje kwa sasa huku pia akipewa pamoja na tiketi za ndege na gari ya kutembelea.

ATOA NENO
Katika ukurasa wake wa Instagram kinda huyo aliandika moja ya ndoto zake kwenye soka ilikuwa siku moja kucheza nje ya nchi na sasa Mungu amefanikisha kutimiza ndoto hiyo kuwa kweli huku akitoa shukrani nyingi kwa viongozi wa Simba kwa sapoti kubwa waliyompa.
“Nachukua nafasi hii kuwashukuru mashabiki wote wa Simba, benchi la ufundi, MO Dewji, Mtendaji Mkuu wa wa Simba, Crescentius Magori, Salim Abdallah ‘Try Again’. Nilijiunga Simba na sasa naondoka bado kijana mdogo,” aliandika Salamba.
“Pia, nachukua nafasi hii kuwashukuru viongozi wa Namungo FC japo sijacheza hata sekunde moja, lakini walikubali kuniachia baada ya kupata ofa hii bila kumsahau Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwa kunipa sapoti wakati nilipojiunga na timu hiyo.”