Lampard majanga, mastaa wanane majeruhi Chelsea

Muktasari:

Waingereza Ruben Loftus-Cheek na Callum Hudson-Odoi kwa muda mrefu wamekuwa kwenye orodha ya majeruhi katika kikosi hicho cha Chelsea, huku mmoja Hudson-Odoi akitarajiwa kurudi uwanjani mwisho wa mwezi huu na mwingine Loftus-Cheek hadi Novemba.

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa Chelsea, Frank Lampard amekumbwa na pigo zito baada ya mastaa wake wanane kutarajia kukosa mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Wolves utakaopigwa baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Beki wa kushoto Emerson Palmieri ni staa aliyeongezeka kwenye orodha hiyo ya wachezaji majeruhi kwenye chumba cha wagonjwa huko Stamford Bridge. Emerson alipata maumivu ya misuli dakika ya nane tu katika mechi ya Italia dhidi ya Finland.
Waingereza Ruben Loftus-Cheek na Callum Hudson-Odoi kwa muda mrefu wamekuwa kwenye orodha ya majeruhi katika kikosi hicho cha Chelsea, huku mmoja Hudson-Odoi akitarajiwa kurudi uwanjani mwisho wa mwezi huu na mwingine Loftus-Cheek hadi Novemba.
Kiungo N'Golo Kante naye ni majeruhi, huku The Blues ikitarajia kumkosa pia beki Antonio Rudiger katika mechi itakayopigwa uwanjanni Molineux.
Beki wa kulia kinda Reece James anasumbuliwa na maumivu ya mguu, wakati kiungo Pedro ana tatizo la misuli huku Mateo Kovacic naye akiuguza maumivu ya kisigino. Chelsea wapo pointi mbili tu juu ya lile shimo la timu zinazoweza kushuka daraja.
Mechi 5 zijazo za Chelsea
Sept 14 vs Wolvs - ugenini
Sept 17 vs Valencia - nyumbani
Sept 22 vs Liverpool - nyumbani
Sept 25 vs Grimsby/Macclesfield - nyumbani
Sept 28 vs Brighton - nyumbani