Aussems ampika Kanda kubeba mikoba ya Bocco kwa Mtibwa Sugar

Muktasari:

Mbelgiji huyo alisema majeruhi Bocco yanamfanya awe na uhaba wa washambuliaji, hivyo ameamua kumfanyisha Kanda mazoezi ya peke yake ili aweze kucheza vizuri katika mechi na Mtibwa Sugar.

Dar es Salaam.Kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems bado anahaha kusaka kuliziba pengo la mshambuliaji wake John Bocco anayesumbuliwa na majeraha.

Aussems alitumia muda mwingi wa mazoezi ya leo asubuhi kwenye viwanja vya Gmykhana, kumuandaa mkongwe Deo Kanda kuzipa pengo la Bocco katika mchezo wa Ijumaa wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.

Katika mazoezi hayo Kanda amefanya mazoezi na wenzake awamu mbili ya viungo na stamina, baadae akahamia kwenye mbio akiwa chini ya kocha wa viungo Aden Zran.

Baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Aussems alisema sababu ya Kanda hakumaliza mazoezi tofauti na wenzake.

Mbelgiji huyo alisema majeruhi Bocco yanamfanya awe na uhaba wa washambuliaji, hivyo ameamua kumfanyisha Kanda mazoezi ya peke yake ili aweze kucheza vizuri katika mechi na Mtibwa Sugar.

"Akifanya mazoezi magumu anaweza akaumia mazoezini na mbele kuna mechi na Mtibwa Sugar, pia Meddie Kagere alikuwa na timu yake ya taifa, bado hajafika sijajua ufiti wake upoje ndio maana namuandaa Kanda mapema."

"Tunahitaji ushindi kwenye mchezo huo ndio maana nipo makini na kikosi kuhakikisha wachezaji hawapati majeraha kupitia mazoezi, vinginevyo tupo vizuri na tayari kwa mchezo," alisema Aussems.

Simba mbali ya kumkosa nahodha wao Bocco, katika safu ya ushambuliaji majeruhi mwengine ni Mbrazili Wilker da Silva, ambaye tangu amesajiliwa na kikosi hiko hajacheza hata mchezo mmoja hapa nchini. 

Wilker aliumia akiwa na kikosi hiko Afrika Kusini ambapo walikuwa wakijiaandaa na msimu huu na mpaka sasa licha ya kufanya mazoezi na wenzake, lakini anafanya yake pembeni binafsi huku akiendelea kupata matibabu kutoka kwa daktari wa misuli Paul Gomez.