Makonda atimiza ahadi yake ampa Kaseja Sh10milioni

Muktasari:

Hii ni mara ya pili kwa Makonda kutoa kiasi hicho cha fedha aliwahi kufanya kwa kipa wa Simba, Aish Manula

Dar es Salaam.Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametimiza ahadi yake kwa kumkabidhi kipa namba wa Taifa Stars, Juma Kaseka fedha Sh 10 milioni.

Kaseja alikuwa shuja jana baada ya kuokoa penalti moja na kuisaidia Stars kushinda kwa penalti 3-0 dhidi ya Burundi katika mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.

Baada ya Kaseja kucheza penalti hiyo, Makonda aliandika katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram kuwa kipa huyo kwake ni mchezaji bora.

Katika mchezo huo uliokuwa wa marudiano Stars wakiwa nyumbani timu zote zilimaliza dakika 90 zikifungana bao 1-1 sawa na matokeo ya mchezo wa kwanza kule nchini Burundi kisha kuongezwa dakika 30 ambazo bado matokeo hayakubadilika na kulazimika kwenda kwenye matuta huku Stars wakipata penalti tatu na Burundi wakikosa zote.

Mbali na kumtangaza hivyo pia Makonda aliandika hapohapo kuwa kwa kiwango hicho leo atamkabidhi kiasi cha Sh10 milioni kama zawadi kwa kazi aliyoifanya.

Leo mchana Makonda alimuita Kaseja ofisini kwake akiambatana na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, kaimu kocha mkuu wa Stars, Ettiene Ndayiragije na baadhi ya wachezaji wa Stars, Adi Yusuf, Himid Mao na Boniface Maganga na kumkabidhi kiasi hicho.

Mara baada ya kukabidhiwa fedha hizo mbali na kushukuru Kaseja amesema fedha hizo zitamsaidia katika kusongesha gurudumu la maisha.