Nyota wa Brazil waliocheza na Gerson Fraga wa Simba

Muktasari:

Kwa sasa Gerson ametua kwenye kikosi cha Simba huku akionekana kusuasua kuingia moja kwa moja kwenye mfumo wa Kocha Patrick Aussems.

Dar es Salaam. MWAKA 2007, Brazil ilimteua kijana wa miaka 15, Gerson Fraga Vieira kutoka akademi ya klabu ya Gremio kuwa nahodha wa timu ya taifa chini ya miaka 16.
Mwaka mmoja baadaye klabu ya Gremio ikamteua kuwa nahodha wa timu yao ya vijana wa chini ya miaka 18.
Mwaka 2008, Brazil ikampandisha kijana huyo kuwa nahodha wa timu ya taifa chini ya miaka 17.
Ikiwa na nyota wakubwa leo kama Neymar, Coutinho na Casemiro, timu hiyo ilishinda Copa Amerika U-17 mwaka 2009 na ikashiriki Kombe la Dunia mwaka huo nchini Nigeria.
Akitokea akademi ileile iliyomwibua Ronaldinho Gaucho, Fraga aliyezimudu vyema nafasi za ulinzi wa kati na kiungo wa ulinzi alitabiriwa mambo makubwa.
Japo Brazil si maarufu sana kwa kuzalisha walinzi, lakini ilionekana akademi ya Gremio imevumbua Ronaldinho mwingine.


Vilabu vikubwa vya Ulaya kama vile Villareal, Liverpool na Barcelona vikaanza kupigana vikumbo kumuwania.
Msaka vipaji wa Real Madrid, Julen Lopetegui alimpendekeza kijana hiyo kwa kocha wakati huo, Bernd Schuster.
Hata hivyo, Gremio ilikataa ofa zote ikiwa na ndoto za kumuuza kwa bei kubwa zaidi hapo baadaye.
Wakati yeye akibaniwa na klabu yake, wenzake wakaruhusiwa na vilabu vyao kuondoka zao kusaka maisha mapya. Casemiro ambaye alikuwa Sao Paulo akaenda Real Madrid ilhali Coutinho aliyekuwa Vasco da Gama akaenda Inter Milan ya Italia.
Kwa sasa Gerson ametua kwenye kikosi cha Simba huku akionekana kusuasua kuingia moja kwa moja kwenye mfumo wa Kocha Patrick Aussems.
Hapa Mwanaspoti linakuchambulia walipo mastaa wenzake aliowaongoza kweye kikosi cha timu ya vijana ya Brazil wakati huo akiwa nahodha.

ALISON BECKER - LIVERPOOL
Huyu ni kipa wa klabu ya Liverpool aliyekuwa  miongoni mwa wachezaji waliocheza na kiungo wa Simba, Gerson wakiwa na umri wa miaka 17 katika timu ya taifa ya Brazil iliyoshirki Kombe la Dunia la vijana lililofanyika mwaka 2009 nchini Nigeria.
Baada ya hapo, Alison alichanguliwa tena kwenye kikosi cha vijana wenye umri wa miaka 21, lakini ikawa tofauti kwa Gerson ambaye hakuchaguliwa tena katika kikosi hicho.

NEYMAR-  PSG
Aliwahi kuwa sehemu ya wachezaji waliounda kikosi cha wachezaji wenye umri wa miaka 17 Brazil. Nyota huyu wa PSG alikuwa timu moja na Gerson  ambapo hata hivyo kikosi hicho hakikucheza kwa mafanikio.
Neymar alipandishwa mpaka kikosi cha vijana wenye umri wa miaka 20, lakini kwa upande wa Gerson safari iliishia hapo na kuendelea kuitumikia klabu yake ya Gremio ya nchini kwao.

PHILLIPE COUTINHO- BAYERN
Kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa uwanjani aliwahi kucheza na Gerson kipindi cha ujana wao kwenye kikosi cha vijana wenye umri wa miaka 17 Brazil. Coutinho alikuwa ni miongoni mwa waliotengeneza kikosi cha kwanza cha timu hiyo na kushiriki Kombe la Dunia la vijana nchini Nigeria. Kipindi hicho kiungo huyo alikuwa anakipiga Inter Milan.


CASEMIRO-
REAL MADRI
Panga pangua kiungo huyo mkabaji alikuwa hakosekani kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo na wakati huo alikuwa anahakikisha beki wake, Gerson hapati mshikemshike wowote kutoka kwa wapinzani.
Umahiri wa Casemiro ulikuwa mkubwa na hali hiyo ilifanya timu hiyo ya vijana kuonekana imara zaidi katika eneo la kati kwa kushirikiana na Coutinho.



ZEZINHO-PARANA
Kiungo huyo mtukutu wa klabu ya Parama ya Brazil alikuwa ni mbishi katika suala la kupitwa kirahisi na alikuwa na uelewano mzuri na beki Gerson.
Ubora wa kikosi chao cha vijana ulijengwa na viungo Zezihno, Casemiro na Coutinho ambaye miaka miwili nyuma alikuwa Liverpool.

SIDIMAR
CIGOLINI-TUPA FC
Huyo alikuwa nyota wa zamani wa Atletico Mineiro akiwa pacha mzuri wa Gerson na alikuwa akitengeneza ubora wa sehemu ya ulinzi wa kati akishirikiana na kiungo huyo wa Simba mwenye uwezo pia wa kucheza beki.
Licha ya kwamba Sidimar hakufanikiwa kuwika na kucheza  miongoni mwa timu kubwa, uwezo wake umebaki kuwa juu mpaka leo pamoja na kuisaidia timu yake ya Tupa FC ya nchini kwao Brazil.

CRYSTIAN
SOUZA- NOVO HORIZONTE GO
Alipata bahati ya kucheza na Neymar mara mbili, alikuwa sehemu ya kikosi cha vijana wenye umri wa miaka 17 akiwa na Gerson ambaye walitengeneza safu nzuri ya ulinzi wakati huo.
Crystian baada ya kucheza timu ya vijana alisajiliwa na Santos ya nchini kwao ambako pia alikutana na staa wa PSG, Neymar na baadaye beki huyo aliondoka na kwenda Botafogo kwa mkopo kisha Paulista zote za nchini humo.

JOSE RIBEIRO-CRUZEIRO
Beki huyo kisiki wa kushoto pengine unaweza kusema ni miongoni mwa vijana wa kizazi cha akina Gerson ambaye aliwahi pia kuchezea timu kubwa Ulaya ya AS Roma ya Italia na pia alicheza na Gerson wa Simba.
Jose maarufu kama ‘DODO’ alikuwa ni sehemu ya kikosi cha kwanza cha Brazil cha vijana wenye umri wa miaka 17, na alishiriki Kombe la Dunia kwa vijana lililofanyika Nigeria.

GUILHERME GUSMAO- FLUMINENSE
Kiungo mshambuliaji huyo ambaye anasifika kwa kufunga nje ya box alikuwa miongoni mwa wachezaji waliocheza na Gerson katika kipindi chao cha ujana wakiwa Brazil.
Alikuwa ni mchezaji aliyesifika kwa upole na nidhamu akiwa ndani na hata nje ya uwanja. Kiungo huyo aliwahi pia kucheza CSKA Moscow ya Urusi akitokea Dymamo Kyve ya Ukraine.

FELIPE DA SILVA-AL MUHARAQ FC
Mshambuliaji wa PSG, Neymar alikuwa akijivunia kucheza pamoja na mshambuliaji huyo kutokana na uelewano mzuri wa safu ya ushambuliaji walioutengeneza kwa kipindi hicho.
Mshambuliaji huyo alikuwa akiunda kikosi cha kwanza kikiwa na beki wa kati, Gerson. Mshambuliaji huyo anayekipiga Al-Muharaq ya Bahrain kwa mkopo aliwahi pia kucheza kikosi cha vijana wenye umri wa miaka 15 na beki huyo.

NYOTA WENGINE
Miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakiunda kikosi cha Brazil cha vijana wenye umri wa miaka 15 akiwemo na mchezaji wa Simba, Gerson ni Giovan, Willen, Wellington Da Silva, kwa upande wa washambuliaji.
Mabeki ni Romario Leiria na Romario ilhali kwa viungo ni Joao Pedro, Elivelton na makipa ni Luis Guilherme na Adre.

FRAGA AFUNGUKA
Akizungumzia safari yake katika soka, Gerson anasema ulikuwa ni mwanzo mzuri wenye kumbukumbu nyingi kwenye kazi yake ambapo alipata nafasi ya kuwaongoza Neymar na mastaa wengine kibao ambao kwa sasa wanatamba barani Ulaya. “Nikikumbuka naishia kucheka na kutabasamu. Hakuna anayeweza kuijua kesho yake, ndicho kilichotokea, nimebaki kujivunia kwamba nilicheza nao, siwezi kusema kwamba kuna sehemu nilijikwaa, kila mtu alipangiwa ni kwa namna gani atapata mafanikio,” anasema.


“Nadhani wanaweza kunikumbuka kama tukionana kwa sababu nilikuwa nina sauti mbele yao, najivunia kuona wamepiga hatua, walikuwa wasikivu.”
Nyota huyo anasema licha ya wenzake kupiga hatua na kwenda kucheza soka Ulaya, hajutii kujiunga na Simba.
Juni 25, Simba walitangaza kupitia ukurasa wao wa Instagram kumsajili mchezaji huyo kwa mktaba wa miaka miwili akitokea ATK ya Ligi Kuu India. Gerson ni Mbrazil wa tatu Msimbazi wengine wakiwa ni Tairone Santos na Wilker Henrique.