EXTRASPESHO: Nandy, Aslay, Kiba, Mondi acha muvi iendelee

Muktasari:

Wakati Nandy na Billnass wakitamba na ngoma yao ya ‘Bugana’, mkali mwingine wa Bongofleva, Aslay akishirikiana na Ali Kiba wameachia ngoma moja matata sana iitwayo ‘Bembea’.

NANDY na bebi wake Billnasa a.k.a Billnenga walitawala mitandao yote ya kijamii kutokana na bonge la intavyuu walilopiga na Millard Ayo wakianika kila kitu ambacho kilikuwa hakijazungumzwa kuhusu uhusiano wao.
Walibainisha jambo ambalo halikuwa likifahamika kwa wengi kumbe wapenzi, tena waliopendana sana.
Ukiacha video ile iliyovuja ikiwaonyesha wawili hao wakiwa kitandani, haikuwa ikifahamika sana kama nyota hao wa Bongo Fleva walipata kuwa wapenzi tena waliozama kila mmoja kwa mwenzake.
Video ile ilitafsiriwa tofauti kutokana na usiri uliokuwapo wa uhusiano wao. Wengine waliamini ilikuwa ni video iliyotengenezwa maalum na ‘kuvujishwa kwa makusudi’ kwa ajili ya kuwapa ‘busti’ wahusika. Kwamba waliamua kutumia mbinu chafu kujitangaza zaidi.
Ndio. Katika maisha haya ya stresi nyingi za maisha, vitu vya kijinga ndivyo hupata umaarufu mkubwa.
Na ndivyo alivyopata umaarufu Kim Kardashian wa Marekani. Ilivuja video ya chumbani akifanya ya faragha na msanii Ray J, yule mdogo wake Brandy Norwood.
Ilikuwa video chafu lakini iliyomtangaza Kim dunia nzima. Hivi sasa akiwa ni mke wa rapa Kanye West, Kim anapiga pesa kwenye mambo mengine tofauti.
Hakufanya kitu sahihi Kim. Lakini ilipovuja video ya chumbani ya Nandy na Billnass, wengine waliamini kwamba wawili hao walikuwa wanatafuta kiki ya majina yao. Kwamba pengine ingewatangaza japo robo tu ilivyomtangaza Kim Kardashian duniani.
Walikuwapo pia waliodhani video ilivuja kwa bahati mbaya. Kwamba ilirekodiwa na wasanii wawili ambao pengine walikuwa washapata ‘vitu vyao’ na wakajisahau katika yale maisha yanayozungumzwa sana ya mastaa ya kujirusha  kimaisha na kimahusiano (wao kwa wao na wao na wasio mastaa).
Lakini vyovyote iwavyo. Iwe video ilivujishwa kwa makusudi ama ilivuja kwa bahati mbaya, ukweli unabaki palepale kwamba ilichangia kuwapa umaarufu wawili hao nje ya vipaji vikubwa vya muziki walivyonavyo.
Na intavyuu ile na Millard ilithibitisha kilichoonekana katika video ile hakikuwa maigizo wala tukio la ‘usiku mmoja’, bali iliwaonyesha watu wawili wanaopendana.
Yote hayo kuhusu kupendana kwao yalibainishwa na wawili hao wenyewe wakati wakiipigia ‘promo’ ngoma yao mpya ya pamoja ya ‘Bugana’.
Video yao ile faragha ilisaidia kuwatangaza wao kama wasanii na sasa intavyuu ya maisha yao ya faragha imesaidia kuitangaza ngoma yao ya ‘Bugana’.
Yanayotokea katika gemu ya Bongofleva yanathibisha ushindani uliopo. Kutoa ngoma kali, kuifanyia video kali na kuipigia promo kali. Yote hayo yanaakisi kwenye kupata mkwanja mrefu. Wasanii ambao ngoma zao zinaangaliwa zaidi kwenye YouTube wanapiga pesa nzuri tu kutokana na matangazo yanayowekwa juu ya video zao.
Na ngoma kali zinachochea ushindani katika game na katika kutrend kwenye YouTube.
Wakati Nandy na Billnass wakitamba na ngoma yao ya ‘Bugana’, mkali mwingine wa Bongofleva, Aslay akishirikiana na Ali Kiba wameachia ngoma moja matata sana iitwayo ‘Bembea’.
Aslay siyo mtu mzuri mjue. Akiingia mahali lazima awavuruge. Na ndicho kilichotokea. Haraka ngoma yake hiyo imeshika namba moja ya video zinazotrendi Tanzania.
Na wakati Aslay na Kiba wakiongoza trendi, mara paap Diamond Platnumz naye kaachia ‘teaser’ ya video ya wimbo wake mpya ule tuliokudokeza kwa mara ya kwanza kwenye safu hii ya Extra Spesho wiki iliyopita ambao ni remix ya ngoma iitwayo ‘Yo Pe’ ya yule dogo mwenye umri wa miaka 22 aitwaye Innoss B anayetesa hivi sasa nchini DR Congo. Yaani kila uchao, ‘balaa’ jipya linakuja mjini. Kwa ushindani huu Bongofleva, acha muvi iendelee.