Zahera aifananisha Yanga na Barcelona

Muktasari:

Katika mechi ya Yanga dhidi ya Pamba FC ya mjini hapa, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, ukiwa ni mchezo wa kwanza katika ziara ya wababe hao wa Jangwani mkoani Mwanza. Pamba ndio walioanza kupata bao katika dakika 31 lililofungwa na Saady Kipanga, huku lile la Yanga likiwekwa kimiani na David Molinga katika dakika ya 87.

Mwanza. Wakati ikihitimisha tukio la Wiki ya Mwananchi kwa Kanda ya Ziwa jijini Mwanzai, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ameifananisha klabu hiyo na Barcelona ya Hispania, akisisitiza kuwa  watatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu wamejipanga vizuri.
Zahera alisema hata timu za Ulaya hufungwa, lakini mwisho hutangaza ubingwa, hivyo Yanga haitakata tamaa katika mashindano mbalimbali inayoshiriki ikiwamo mchezo wao na Zesco ya Zambia utakaopigwa wiki ijayo ambao utatoa mwelekeo kuelekea hatua ya makundi ya ligi hiyo.
Alisema amesikiliza kwa umakini vilio vya mashabiki wa timu hiyo wanaotaka itinge hatua ya makundi, lakini ahadi yake kwao ni moja tu, watatinga.
Zahera alisema zipo timu barani Ulaya huanza vibaya michezo zinayoshiriki kwa kufungwa, lakini kadri inavyoendelea hujikuta zinamaliza na ubingwa mikononi na ndivyo itakavyokuwa kwao. Yanga ilifungwa bao 1-0 na Ruvu Shooting katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Agosti 28.  
“Mechi moja tu ndio itupotezee ndoto za ubingwa? Barcelona waliwahi kufungwa mechi ya awali kabisa lakini walitangaza ubingwa, kwa hiyo hata sisi Yanga itakuwa hivyo,” alitamba Zahera.
Kocha huyo mwenye ushawishi mkubwa kwa sasa Jangwani, alisema malengo ya timu ni kufuzu kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku hesabu zingine zikiwa za kubeba taji la Ligi Kuu Bara.
Aliwasifia nyota wake akisema kwa sasa wanampa furaha kutokana na jinsi wanavyomwelewa mazoezini na kwamba, mchezo wa Jumamosi dhidi ya Zesco ni lazima wafanye kweli.
“Nashukuru vijana wanaenda vizuri, wananielewa ninachowaelekeza hata ambao hawapo kambini, lakini huko walipo kwenye timu ya Taifa wanafanya mazoezi, kwa hiyo sioni tatizo,” alisema.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msolla aliwaahidi mashabiki wa timu hiyo Kanda ya Ziwa kuwa, iwapo itatinga makundi ya Klabu Bingwa Afrika watahamishia michezo hiyo katika Uwanja wa CCM Kirumba mjini hapa.
Dk Msolla alisema hatua hiyo inatokana na mazingira mazuri ya Jiji la Mwanza ikizingatiwa kwamba mbali na Uwanja wa Taifa, dimba lingine ambalo walijaza kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kulitumia ni lile la CCM Kirumba na kwamba wanaamini wakiwa jijini hapa kila kitu kitakwenda vizuri.
Mwenyekiti wa matawi ya Yanga Mwanza, Saleh Akida alisema wamejipanga kuhakikisha timu hiyo inapata mafanikio inapokuwa mkoani humo.