Ndayiragije, Matola walivyogawana dakika 120 kuongoza mauaji Taifa Stars

Muktasari:

Makocha hao wawili walifanya kitu cha tofauti katika medali ya soka baada ya kubadilisha dakika za kuongoza na kutoa maelekezo kwa wachezaji wa Stars.

Dar es Salaam. Taifa Stars imewapa raha Watanzania, kila unapopita ni furaha, mashabiki waliojitokeza Uwanja wa Taifa kila mmoja aliondoka na tabasamu.

Shangwe na furaha hiyo ni baada ya Taifa Stars kuitoa Burundi kwa penalti 3-0 kufuatia mchezo huo wa kusaka kufuzu kwa hatua ya makundi ya Kombe la Dunia2022 kumalizika kwa sare 1-1 katika dakika 120.

Katika mchezo mtamu, yapo mengi yaliyotokeza kuanzia ndani na nje ya uwanja.

Acha matokeo yaliyopatikana, lakini kilichovutia zaidi ni makocha wa Taifa Stars, Kaimu kocha mkuu Ettiene Ndayiragije na msaidizi wake Suleiman Matola.

Makocha hao wawili walifanya kitu cha tofauti katika medali ya soka baada ya kubadilisha dakika za kuongoza na kutoa maelekezo kwa wachezaji wa Stars.

Mchezo ulikuwa na dakika 120. Dakika 45 za mwanzo aliyekuwa na jukumu la kutoa maelekezo alikuwa ni Matola huku bosi wake, Ndayiragije alikuwa amekaa. Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko matokeo yalikuwa sare bao 1-1.

Katika dakika hizi, Matola kiungo wa zamani wa Taifa Stars na timu ya Simba ambaye sasa ni Kocha wa Polisi Tanzania alikuwa amesimama na kutoa maelekezo ya hapa na pale.

Kipindi cha pili, Ndayaragije alishika usukani wa kuhakikisha anaipeleka mbele Tanzania bila kujali yeye ni mzaliwa wa Burundi.

Hata hivyo, dakika 45 zake hazikuzaa matokeo chanya kwa Stars pamoja na kucheza soka safi, lakini ilishindwa kupata bao.

Kocha huyo ambaye amekuwa na mafanikio tangu alipotua Tanzania katika msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania 2017/18 akikinoa kikosi cha Mbao FC cha jijini Mwanza aliendelea kusimama katika dakika 30 za nyongeza hadi alipohakikisha amewafyeka Burundi kwa mikwaju ya penalti.

Ndayiragije kwa sasa ni kocha wa Azam FC aliyojiunga nayo msimu huu akitokea KMC FC baada ya pambano, alikwenda kusalimiana na benchi la Burundi.

Sijui aliwapo pole na wao kumlaumu kwa kuhakikisha wanatoka? Hilo tuwaachie wenyewe.