Mbona iko hivi: Itakuwa kamari, ila Yondani anaweza

Muktasari:

Tangu wakati huo amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Yanga na Taifa Stars kiasi kwamba wakati yeye na Erasto Nyoni walipotangaza kutaka kustaafu timu hiyo, wamekataliwa kwa sababu hadi sasa hakuna mbadala wao wa maana.

NILIKUWA kiongozi katika Klabu ya Simba wakati Kelvin Yondani alipofanya uamuzi wa kuhamia Yanga akitokea kwa watani wao wa jadi. Bado nakumbuka ilivyokuwa na kusema kweli nitakuwa mtu wa mwisho kumlaumu kwa kufanya uamuzi huo mgumu.
Nadhani tatizo lilikuwa kwamba alikuwa anataka kiasi cha fedha ambacho uongozi wetu wakati huo haukuona kama anastahili. Kuna siku nilikaa na Juma Kaseja, akiwa nahodha wa Simba wakati huo na aliniambia maneno ambayo bado nayakumbuka hata sasa: “Yondani ndiye sentahafu bora wa Tanzania kwa sasa na akiondoka mtajua umuhimu wake”.
Halafu tukasikia kina Seif Magari na Abdallah Binkleb wamemsainisha Yanga. Na tangu wakati huo amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Yanga na Taifa Stars kiasi kwamba wakati yeye na Erasto Nyoni walipotangaza kutaka kustaafu timu hiyo, wamekataliwa kwa sababu hadi sasa hakuna mbadala wao wa maana.
Hivyo, tangu Kaseja aliponiambia ukweli huo kuhusu Yondani, nimekuwa nikimheshimu sana. Naheshimu ukweli kwamba amedumu katika kiwango cha juu katika soka la Tanzania kwa zaidi ya miaka 10 –akicheza katika kiwango cha juu. Hili si jambo la kawaida hapa kwetu kwani mara nyingi muda wa wachezaji wengi kutamba hauzidi miaka mitano kabla mafanikio hayajapanda kichwani. Yondani ni kama betri za Duracell zinazofahamika kwa kudumu muda mrefu.
Jambo ambalo nimeanza kuliona sasa kwa Kelvin; wenzake wanamwita Cotton Juice na hadi leo sijajua kwa nini, ni uwezo mkubwa wa kupiga pasi ndefu kutoka katika safu ya ulinzi. Brazil na Arsenal zina mchezaji anayeitwa David Luiz na nadhani Yondani anaweza kuwa anakaribiana naye kwa uwezo huo.
Kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yaliyofanyika Misri, Yondani, pasi na shaka yoyote, ndiye aliyekuwa mchezaji aliyepiga pasi nyingi za maana kwenda mbele kuliko mchezaji mwingine yeyote wa timu ya taifa.
Kimsingi, kama kulikuwa na tatizo kubwa Misri, basi lilihusu suala la wachezaji kutoa pasi zinazofika kwa mlengwa. Lakini Yondani alikuwa anazipiga tu; kushoto, kulia mbele mita 50 mpaka 60 na zinafika anakotaka.
Nilitazama pia mechi baina ya Stars na Burundi Jumatano iliyopita na bado Kelvin alinivutia kwa pasi zake. Kwenye mechi ile hazikuwa sahihi sana kama nilivyoona Misri lakini angalau alikuwa anajitahidi kuziona pasi ambazo viungo wetu huwa hawazioni.
Himidi Mao, Salum Abubakar na Jonas Mkude ni viungo wazuri kwenye majukumu yao lakini utoaji wa pasi za hatari kwa washambulizi si sifa yao kubwa sana. Sure Boy alikuwa akilalamikiwa sana kwa kupiga pasi za pembeni sana katika miaka ya nyuma lakini sasa naona anaaza kupiga pasi nyingi za mbele lakini bado hajawa wa hatari namna hiyo. Tatizo liko hivyo kwa Mkude na Himidi pia.
Nimeanza kuwa na mawazo kwamba ipo siku atakuja kocha na kumpanga Yondani kama kiungo wa ulinzi na watu wakashangaa. Kuna msemo kwamba mbwa mzee hafundishwi mbinu mpya lakini kama kuna kitu ambacho wachezaji wazuri wanajulikana, basi ni kuweza kujibadili na kucheza nafasi tofauti.
Kwa tatizo hili la wapiga pasi kwenye eneo letu la kiungo, ningemsogeza Yondani mbele kidogo halafu nafasi yake akae mtu kama Abdi Banda (naye ni mzuri wa pasi ndefu pia) au Aggrey Morris au beki mwingine mzuri wa kati wa kucheza na Nyoni kama ambavyo Rafa Benitez aliwahi kumjaribu Luiz pale Chelsea.
Sijui kama kocha mzalendo anaweza kufanya uamuzi mgumu namna hii. Sijui kama mchezaji mwenyewe atakubali kufanya mabadiliko haya ya haraka. Lakini kama ningekuwa kocha, na kwa sababu najua tatizo la pasi kwenye eneo letu la kiungo, ningejaribu kucheza hii kamari.
Faida yake ni kwamba tunaposhambuliwa, Yondani anabadilika na kutengeneza safu ya mabeki watatu wa kati. Kwa hiyo, kwa namna nyingine, ningeweza kujaribu kucheza hiyo kamari.
Ila sijui kama kocha mwenye ‘cojones’ za kujaribu kamari hii.

Kitabu cha Michael Owen
Habari kubwa ya soka nchini Uingereza kwa sasa inahusu kitabu kilichotoka cha mchezaji wa zamani wa kimataifa wa taifa hilo, Michael Owen. Kwenye kitabu hicho cha maisha yake, Owen ameeleza kuhusu ‘bifu’ lake na nyota mwenzake wa zamani wa England, Alan Shearer. Nimeagiza niletewe hicho kitabu na sijakitia mkononi lakini inaonekana ni kitamu balaa.
Katika soka mabifu ni jambo la kawaida. Wakati nilipokuwa kiongozi kwenye mpira wetu, nilikuwa nafahamu kuhusu makundi ambayo hujitokeza miongoni mwa wachezaji. Kuna watu wanacheza pamoja lakini mechi ikiisha hata salamu huwa hawapeani.
Kuna tuhuma za kupigana ‘misumari’, kuna wanaojulikana kwa kupokea ‘mzigo’ kutoka timu pinzani na kuna wale wanaojulikana kwa kutaniwa kwa sababu hadi wamejiunga na timu kubwa walikuwa hawajafanyiwa hata ‘sunna’. Unaweza kucheka mambo mengine.
Hata hivyo, hadithi hizi zinaishia kwenye vijiwe na viambaza vya jamii ya mpira. Si watu wengine wanafahamu nini kinaendelea katika eneo la uhusiano baina ya wachezaji, viongozi na mashabiki wao.
Nadhani kuna fursa kwa waandishi wa Tanzania na wachezaji kuanza kufunguka na kueleza kitu kuhusu maisha yao. Kwa bahati nzuri, ninafahamu wachezaji ambao marafiki zao wakubwa ni wanahabari na huo ni msingi mzuri wa kuanzia.
Vitabu hivi vitakuwa na mafunzo makubwa kwa vijana na wengine ambao watakuwa wanataka kufanya uamuzi wa kujitosa kindakindaki katika mchezo wa mpira na mingine kama ngumi, riadha, kikapu na mingine. Kote huko kuna michapo yake na mambo yanayotakiwa kujulikana lakini hayatakuja kujulikana.
Hii ni fursa. Nani ambaye hatataka kusoma kitabu kuhusu Haruna Moshi Boban halafu humo ndani akaeleza kuhusu mambo yake na Athumani Idd ‘Chuji’ wakati ule wa Taifa Stars ya Marcio Maximo?