Kuna sababu mbili za kuanza na Farid leo dhidi ya Burundi

Muktasari:

Naweza kuelewa kwanini Farid alikaa benchi Bujumbura. Ni kwa sababu tulikuwa ugenini na nafasi yake ilikwenda kwa kiungo mmoja. Hata hivyo, kwa Dar es Salaam leo tunapaswa kwenda na 4-3-3. Tunapaswa kuanza na viungo watatu na watu watatu kule mbele.

NILIWATAZAMA Burundi katika pambano dhidi ya Taifa Stars Jumatano jioni pale Bujumbura sikuwalewa. Hawakuwa wale ambao niliwaona katika michuano ya Mataifa ya Afrika pale Misri.
Waliamka zaidi dakika za mwisho za kipindi cha pili lakini vinginevyo mpira wote ulikuwa umechukuliwa na Taifa Stars ambayo ilikosa bao la wazi katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Simon Msuva. Kipindi cha pili Stars ilijirekebisha kupitia wa Msuva huyohuyo baada ya Burundi kutangulia bao.
Kwanini tuliwatala Burundi? Kunaweza kuwa na sababu mbili. Kwanza kabisa kocha wetu, Ettiene Ndayiragije, ambaye ni raia wao, aliamua kupanga viungo wengi katika eneo la katikati. ‘aliua’ winga zote na kuchezesha viungo watupu.
Aliwapanga kwa pamoja, Jonas Mkude mbele yake akacheza Sure Boy, kushoto akacheza Hassan Dilunga, kulia akacheza Himid Mao. Lengo lake ilikuwa waubane uwanja na kumiliki mpira vema huku Simon Msuva akicheza kati na Mbwana Samatta akitokea pembeni. Wakati mwingine walikuwa wakibadilishana.
Baada ya kuchunguza kilichotokea Bujumbura nadhani kocha wetu, Ettiene, ambaye ni mmoja kati ya makocha ambao nawaheshimu zaidi nchini kwa sasa, anapaswa kumpunguza kiungo mmoja na kumpanga Farid Mussa.
Naweza kuelewa kwanini Farid alikaa benchi Bujumbura. Ni kwa sababu tulikuwa ugenini na nafasi yake ilikwenda kwa kiungo mmoja. Hata hivyo, kwa Dar es Salaam leo tunapaswa kwenda na 4-3-3. Tunapaswa kuanza na viungo watatu na watu watatu kule mbele.
Katika watu hawa watatu, mmoja anaweza kushuka na kutengeneza viungo wanne kwa mara nyingi eneo la katikati. Farid huyuhuyu anakupa vitu viwili akiwa fomu kama ile aliyokuwa nayo Misri. Kwanza ana uwezo wa kukaba na pia ana kasi kubwa ya kwenda mbele na kutengeneza jambo.
Hapa ndio maana  nampigia debe Farid. Tutakuwa nyumbani, tutawachanganya kwa kelele, lakini zaidi ni kwamba tunahitaji kasi zaidi katika kutengeneza mashambulizi. Pengine tungeweza kuwa na kasi zaidi pale Bujumbura lakini uwanja wao haukuruhusu. Uwanja wa nyasi bandia ambao umechakaa unazuia mpira kwenda kwa kasi. Kupitia televisheni zetu tuliweka kuona ‘vimipira’ vilivyojazwa katika nyasi bandia vikurukaruka uwanjani. Ni tofauti na Chamazi.
Eneo jingine ambalo inabidi tulifanyie kazi ni upande wa kulia katika eneo la ulinzi. Haruna Shamte alionekana kuwa mzito. Hatujui kwanini Hassan Kessy hakuanza.  Mchezaji ambaye anaweza kumuweka benchi Kessy kwa sasa na tusilalamike ni Shomari Kapombe. Lakini kama Kapombe hayupo basi tunastahili kwenda na Kessy.
Kila la kheri kwa Taifa Stars. leo nitaeleza jinsi safari ya Qatar inavyoweza kutusaidia kuimarisha kikosi kwa ajili ya Afcon 2021 pale Cameroon. Mpaka wakati huo, twende tukashangilie Stars kwa sasa.