Yanga yawanufaisha waendesha bodaboda Mwanza

UJIO wa Yanga jijini hapa ni kama unawanufaisha wafanyabiashara hasa waendesha bodaboda kutokana na mashabiki wengi kuhitaji huduma ya kupelekwa uwanjani ambako Yanga inafanya mazoezi yake.
Yanga wamepiga kambi yao jiji hapa ikijiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco ya Zambia ambapo kesho Jumamosi itacheza mechi ya kirafiki na Pamba FC uwanja wa CCM Kirumba.
Waendesha bodaboda hao wamesema hiki ni kipindi kizuri kwao kupiga pesa wakati timu ikifanya mazoezi na inapokuwa na mechi kwani mashabiki wanakuwa wengi wanaohitaji huduma ya usafiri huo.
Baada ya mechi hiyo, Yanga itacheza mechi nyingine dhidi ya Toto Africans nayo ya Mwanza Septemba 10 kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waendesha bodaboda hao kutoka Mtaa wa Uhuru wamebainisha kuwa ujio wa Yanga wameupokea kwa mikono miwili kwasababu umewaongezea nafasi ya kuingiza mkwanja.
"Abiria ni wengi kwa sasa, tunategemea mechi ya kesho Jumamosi tutanufaika sana maana wasafiri wanaotumia usafiri wa bodaboda wanaongezeka katika mechi hizi kubwa" amesema Eradius Fransis .
Kwa upande wa Elius Joshua amesema biashara yao ya Bodaboda imeimarika sana kwa kipindi hiki ambacho Yanga wapo jijini hapa na kwamba mambo sio mabaya kwa upande wao hivyo wanategemea wataendelea kunufaika na ujio huo.