Keown ampa Kiatu cha Dhahabu mapema tu Salah

Muktasari:

Staa huyo wa Misri amefunga mabao 57 kwenye Ligi Kuu England tangu alipojiunga na Liverpool akitokea Roma mwaka 2017, alishinda tuzo hiyo ya ufungaji bora katika msimu wake wa kwanza Anfield, alipofunga mabao 32 katika mechi 36.

LONDON, ENGLAND. BEKI wa zamani wa Arsenal, Martin Keown ameweka shilingi yake kwa straika wa Liverpool, Mohamed Salah kwamba ndiye atakayenyakua Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England msimu huu.
Staa huyo wa Misri amefunga mabao 57 kwenye Ligi Kuu England tangu alipojiunga na Liverpool akitokea Roma mwaka 2017, alishinda tuzo hiyo ya ufungaji bora katika msimu wake wa kwanza Anfield, alipofunga mabao 32 katika mechi 36.
Alibeba tena msimu uliopita, lakini safari hii akilazimika kugawana na mastaa wengine Sadio Mane na Pierre-Emerick Aubameyang kutokana na kulingana mabao yao, kila mmoja akifunga mara 22 .
Hadi sasa msimu huu, Mo Salah ameshafunga mabao matatu na jambo hilo linamfanya Keown kuamini kwamba staa huyo wa Liverpool anakwenda kujibebea Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
"Kama Liverpool watakwenda kuwa mabingwa, basi hiyo itakuwa kazi ya Mohamed Salah," alisema Keown.
"Atamfunika sana Sadio Mane msimu huu. Salah alikuwa na wakati mgumu msimu uliopita, lakini umeona jinsi kila alichokifanya."
Wakati Keown akiamini hilo, straika zamani wa Blackburn na Celtic, Chris Sutton anaamini staa wa Tottenham, Harry Kane ndiye mchezaji atakayemaliza akiwa kinara wa mabao kwenye ligi. Kane alishinda tuzo hiyo katika msimu wa 2015-16 na 2016-17.
Kwa sasa, straika wa Manchester City, Sergio Aguero ndiye anayeongoza kwa mabao baada ya kufunga mara sita msimu huu.