Maguire awaambia wenzake tulieni, acheni papara

Muktasari:

Ni presha kubwa kwa Kocha Ole Gunnar Solskjaer baada ya kikosi chake kupoteza tena uongozi wao wa uwanjani na hivyo kushindwa kutoka uwanjani na pointi zote tatu katika mechi mbili mfululizo ambazo walitangulia kufunga.

MANCHESTER, ENGLAND. BEKI ghali duniani, Harry Maguire amewaambia wachezaji wenzake huko kwenye kikosi cha Manchester United wajiamini pindi wanapokuwa na mpira miguuni baada ya kuona makosa mengi katika mechi ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Southampton kwenye Ligi Kuu England Jumamosi iliyopita.
Ni presha kubwa kwa Kocha Ole Gunnar Solskjaer baada ya kikosi chake kupoteza tena uongozi wao wa uwanjani na hivyo kushindwa kutoka uwanjani na pointi zote tatu katika mechi mbili mfululizo ambazo walitangulia kufunga.
Kwenye mechi dhidi ya Southampton, Daniel James aliitanguliza Man United kwa bao matata kabisa, lakini mambo yalikuja kutibuka kwenye kipindi cha pili, ambapo Jannik Vestergaard akawasawazishaia Saint.
Man United ilipoteza pia uongozi kwenye mechi ya sare dhidi ya Wolves, kabla ya kuchapwa na Crystal Palace.
Beki Maguire aliyenaswa kwa Pauni 80 milioni alisema Man United ilikuwa hovyo uwanjani, hivyo wanapaswa kuboresha viwango vyao baada ya kuambulia pointi tano tu katika mechi nne.
“Ni mechi nyingine tuliyostahili kushinda. Tulitengeneza nafasi nyingi sana, lakini matokeo yake tumepoteza pointi mbili. Jinsi tulivyoanza mechi ya kwanza kwenye msimu ilipaswa kuwa hivyo. Tulistahili kushinda dhidi ya Wolves tukafeli, kisha tukaja kuruhusu mashuti mawili ya Palace na wakatufunga mara mbili. Tunapaswa kuutendea haki mpira. Tumekuwa tukipoteza sana mpira uwanjani, tunaharibu, yatupasa kujiamini tunapokuwa na mpira.
“ Sisi ni Man United, tunapaswa kumiliki mchezo. Muda ambao tutashindwa kutawala mchezo, tutaadhibiwa."
Licha ya kwamba beki wa Southampton, Kevin Danso alitolewa kwa kadi nyekundu dakika 73, Man United bado ilishindwa kutumia nafasi hiyo kupata ushindi muhimu.
MECHI 5 ZIJAZO ZA UNITED
Sept 14 vs Leicester City - nyumbani
Sept 19 vs Astana - nyumbani
Sept 22 vs West Ham – ugenini
Sept 25 vs Rochdale - nyumbani
Sept 30 vs Arsenal - nyumbani