Zahera aishangaa sheria ya mavazi kwa makocha

Muktasari:

Sheria mpya ya mavazi kwa benchi la ufundi kwa klabu imelenga Ligi Kuu, daraja la kwanza na la Pili imetolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ameshangazwa na kanuni mpya ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ya kumtaka kocha wa timu za Ligi Kuu kufuata taratibu za mavazi na kuweka wazi kuwa duniani kote hajawahi kushuhudia sheria ya mavazi.

Marekebisho hayo ya Ligi Kuu 2019/20 yalitolewa Agosti 21, kanuni ya 14 kipengele cha 2m kinaeleza kuwa kocha mkuu na viongozi wa benchi la ufundi wanawajibika kuvaa sare maalum kwa timu yao kwa benchi la ufundi.

Kipengele hicho kinaendelea kueleza kuwa endapo kocha mkuu atahitaji kuvaa mavazi mavazi tofauti, anawajibika kuwa katika mavazi ya heshima na nadhifu, ikisisitiza kuwa ukiukwaji wowote utavutia adhabu kwa mhusika.

Zahera alisema sheria zinawekwa ili zifuatwe hivyo hana budi kukinzana na TFF atafanya kama inavyotakiwa huku akisisitiza kuwa jambo hilo ni jipya kwake tangu ameanza kujihusisha na mpira.

"Duniani kote katika soka hakuna sheria ya mavazi kuwa kocha anatakiwa avaaje, wengi wanavaa kulingana na namna wanavyojisikia, lakini kwakuwa ni utaratibu ambao umewekwa maalumu ni muhimu kufuatwa nitafanya kama wanavyotaka," alisema na kuongeza kuwa.

"Nguo nilizokuwa navaa hakuna mtu aliyekuwa ananipangia nilikuwa navaa kawaida na nilikua najihisi vizuri kama shida ni suti nitavaa sana kwani ninazo pia tukutane michezo ijayo," alisema Zahera.