Kogalo yachungulia makundi Ligi ya Mabingwa

Muktasari:

Waarabu hao waliowatupa nje Sonideep wa Nigeria watawaalika Gor Septemba 13-15 kisha baada ya wiki mbili waweze kurudiana Nairobi.

KUNA uwezekano mkubwa Gor Mahia wakatinga hatua ya makundi kwenye dimba la CAF Champions League kiulani bila ya kushiriki mechi za mchujo wa raundi  ya pili.
Ishu ipo hivi, baada ya kuwang’oa Waburundi Aigle Noir kwenye mchujo wa raundi ya kwanza, wameratibiwa kukutana na Waarabu USM Alger raundi ya pili ya mchujo huku anayefanikiwa kumbwaga mwenzake, basi anatinga hatua ya makundi ya dimba hilo msimu huu.
Hata hivyo, kwa namna hali ilivyo sasa , Gor wanaweza kuteleza kiulaini hadi kundini baada ya Waarabu hao kusema wamesota kinoma na huenda wakajiondoa kwenye mashindano hayo.
Akifunguka hivi majuzi, Katibu wa klabu hiyo, Mounri Debichi aliviambia vyombo vya habari kwao klabu yao inahitaji tukio la dharura litakalowakwamua kutoka kwenye hali yao hiyo mbaya ya kifedha.
Waarabu hao waliowatupa nje Sonideep wa Nigeria watawaalika Gor Septemba 13-15 kisha baada ya wiki mbili waweze kurudiana Nairobi.
Kusota kwa USM Alger kulianza Juni mwaka huu baada ya kukamatwa kwa mdhamini wao mkuu mfanyabiashara bwanyenywe Al Haddad aliyekuwa sapota mkuu wa Rais aliyeng’olewa madarakani Abdelaziz Boutefika.
Al Haddad anashtumiwa kwa kumiliki pasipoti za mataifa mawili pasi na kuitaarifu serikali yake jinsi inavyotakiwa kisheria. Vile vile anashtumiwa kwa kasfha kadhaa za ufisadi.
Ingawaje hali hiyo inaweza kuwa Baraka kubwa kwa Gor Mahia, nao vile vile wanapitia hali ya msoto kufuatia kujiondoa kwa mdhamini mkuu Sportpesa.