Mkongwe Oliech azaua balaa jipya Gor Mahia

Sunday September 1 2019

Mkongwe Oliech, azaua balaa, jipya Gor Mahia, Mwanaspoti, Tanzania, Kenya

 

By THOMAS MATIKO

BAADA ya kuvunjiwa mkataba na Gor Mahia kwa utovu wa nidhamu huku uongozi ukisema hautaki kumwona tena, straika Dennis Oliech kwa upande wake kasisitiza bado ni mchezaji wa klabu hiyo.
Juzi kati, uongozi wa Gor ulimwandikia barua ukimfahamisha umeamua kuvunja mkataba wake nao kutokana na  tabia yake ya kuendelea kususia mazoezi bila ya kutoa maelezo kwa kocha au kiongozi yeyoye yule wa klabu.
Gor ilisema hata licha ya kumsaka kwa njia za simu mara kwa mara, Oliech hakuwa akizipokea hivyo kuwangeweza kuendelea naye.
Kigezo kingine cha kumchuja ni taarifa straika huyo alikuwa amejitosa kwenye siasa za ugombeaji wa kiti cha Ubunge cha Kibra.
Hata hivyo, Oliech kajibu mapigo akiipuuzilia mbali barua hiyo kwa kusisitiza bado angali mchezaji wa Gor.
“Hizi stori mnazozisikia zote ni uwongo mtu. Ukweli wa mambo, bado sijapona jeraha nililopata baada ya kuteguka mkono wangu, hata bendeji imeondolewa wiki mbili zilizopita.
“Kuhusu simu, timu meneja amenipigia mara mbili tu kinyume na inavyosemwa na hata kama sikupokea kwa  nini hakutuma ujumnbe. Gor nimefanya nayo mazoezi mara  mbili tangu wamerudi kutoka Burundi. Baadaye daktari akanishauri nijiepushe na mazoezi kwa mpaka nitakapopona, meneja wa timu anaifahamu hilo” Oliech kajitetea.
Oliech sasa anaishutumu Gor kwa kutokuwa mvumilivu naye mpaka atakapopona. Vile vile kadai suala la siasa linatumiwa dhidi yake kutokana na harakati zake za kutetea maslahi ya wachezaji wenzake hasa kwenye ucheleweshaji wa mishahara yao.
Hata hivyo, kwa upande wa Ofisa Mkuu Mtendaji wa Gor Omondi Aduda alisema Oliech anachofanya ni kuibua mavipindi tu ila ukweli wa mambo, hawamhitaji kutokana na tabia zake hizo chwara kama zilivyoelezewa.
“Tumechoka naye mzee hatua atakayochukua baada ya hapo wala haituhusu sisi. Huwezi kuendelea kuwa mwajiri wako nikiwa nimekuvunjia mkataba.
“Hizi ishu zote anazoibua hazina maana kwa sasa, ni mavipindi tu, tulikuwepo na muda wa kuzitatua ala akawa anakwepa” Aduda kasisitiza.
Oliech alikuwa kwenye mkataba wa miaka miwili uliokuwa ukimlipa Sh300,000 kila mwezi.

Advertisement