Kazi ipo! Pogba apewa tena kazi ya kupiga penalti Manchester United

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA Ole Gunnar Solskjaer amesema sasa anamruhusu tena Paul Pogba kupiga penalti baada ya Marcus Rashford aliyekuwa akimwaamini kukosa mkwaju wake dhidi ya Crystal Palace kwenye Ligi Kuu England Jumamosi iliyopita.
Rashford ameigharimu Man United na kuchapwa 2-1 katika mchezo huo uliofanyika Old Trafford, huku ukiibua mjadala mzito kuhusu upigaji wa penalti wa mastaa hao wa Solskjaer.
Pogba alikosa penalti yake ya nne kati ya 11 alizopiga wakati Man United ilipotoka sare ya 1-1 dhidi ya Wolves kwenye Ligi Kuu England wiki iliyopita, lakini Rashford alifunga dhidi ya Chelsea kwenye mechi ya kwanza ya ushindi wa 4-0 kwenye wiki ya kwanza ya msimu, kabla ya kuja kukosa Jumamosi na kuigharimu timu yake.
Kocha Solskjaer alisema hadharani baada ya Pogba kukosa huko Molineux kwamba Man United bado itaendelea kuwa na wapiga penalti wawili kwa maana ya kiungo huyo Mfaransa na Rashford. Lakini, mashabiki na wachambuzi wa soka walipingana naye na kumtaka Pogba asiwekwe kwenye orodha ya wapiga penalti. Baadhi ya wachezaji wa Man United walionekana kusitasita kuhusu Pogba na kutaka Rashford ndio awe chaguo la kwanza kwenye kupiga penalti.
Lakini, sasa baada ya Rashford kukosa penalti yake dhidi ya Palace, kocha Solskjaer sasa amebadili mawazo yake.
"Wachezaji wote wanajiamini na ni wapiga penalti wazuri. Mimi mwenyewe nilishawahi kuwa kwenye hali kama hiyo, nilikosa penalti Norway," alisema.
"Kunapokuwa na majira mawili, basi kuna mmoja atakuwa anajiamini zaidi. Na Pogba amefunga nyingi sana huko nyuma, hivyo sio tatizo."