Jjuuko aisubiri Simba tu atue Wydad Casablanca

Muktasari:

Jjuuko amefuzu vipimo vya afya tangu Ijumaa na sasa anasubiri barua ya kumruhusu kutoka Simba pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumpatia ITC ndani ya saa 48.

Dar es Salaam.Beki Uganda Cranes, Murushid Jjuuko amefuzu vipimo vyake vya katika klabu ya Wydad Casablanca, Morocco sasa anaisubiri Simba kumpa barua ya kumuachi tu.

Jjuuko alikwenda Morocco akitokea Entebbe (Uganda) katika ya wiki hii kwa ajili ya kukamilisha suala la vipimo vyake vya afya ili kukamilisha uhamisho huo.

Kwa mujibu wa wakala wa mchezaji huyo, Jjuuko kwa sasa yupo katika majadiliano kuhusu maslahi yake binafsi kabla ya kusaini mkataba wake wa miaka mitatu.

‘Kwa sasa anachosubiri ni kupata kibali kutoka kwa Simba ya Tanzania ambako mkataba wake umebakia siku 60 kabla ya kumalizika,” alisema wakala huyo.

“Jjuuko amefuzu vipimo vya afya tangu Ijumaa na sasa anasubiri barua ya kumruhusu kutoka Simba pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumpatia ITC ndani ya saa 48.”

Kabla ya kwenda Morocco, Jjuuko alikuwa akijihusisha na uchezaji wa gofu Entebbe Golf Club akiwa na rafiki zake wa zamani wa shule pamoja na mchezaji mwezake wa Uganda Cranes, Denis Iguma.

Wydad Casablanca ni moja ya timu yenye mafanikio nchini Morocco ikiwa na mataji 48.

Jjuuko ameichezea Uganda katika fainali mbili za Mataifa ya Afrika Gabon (2017) pamoja na fainali za Misri (2019).