Simba imekwama hapa tu kwa UD Songo

Muktasari:

Simba msimu uliopita iliweka rekodi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, lakini mambo yamekuwa tofauti msimu huu baada ya kuondolewa na Songo katika hatua ya awali kwa sheria ya bao la ugenini baada ya mechi ya kwanza kumalizika kwa suluhu jijini Maputo

Dar es Salaam. Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, imeanga mashindano ya Ligi ya Mabingwa mapema baada ya kulazimisha sare 1-1 na UD Songo nyumbani.

Beki Erasto Nyoni alifunga bao la kusawazisha kwa Simba katika dakika 87 kwa mkwaju wa penalti, baada ya UD Songo kufunga bao la mapema dakika ya 13 kupitia Luiz Misquissone.

Simba msimu uliopita iliweka rekodi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, lakini mambo yamekuwa tofauti msimu huu baada ya kuondolewa na Songo katika hatua ya awali kwa sheria ya bao la ugenini baada ya mechi ya kwanza kumalizika kwa suluhu jijini Maputo.

Katika mchezo huo Simba ilipigwa na butwaa baada ya wapinzani wao UD Songo kuanza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza katika dakika 13 kwa mpira wa adhabu uliopigwa na Misquissone uliokwenda moja kwa moja wavuni.

Kocha mkuu wa Simba, Patrick Aussems aliingia na kikosi kikiwa na wachezaji wengi wenye uwezo wa kushambulia, lakini walishindwa kuwa makini katika kumalizia nafasi nyingi walizotegeneza.

Aussems katika nafasi ya kiungo ushambuliaji aliwaanzisha Deo Kanda, Francis Kahata ambao walikuwa hawakabi, huku katika upande wa ushambuliaji akimuanzisha Meddie Kagere na Clatous Chama.

Kahata na Kanda walikuwa wazuri pindi wanapomiliki mpira tu huku wanapokuwa wanashambuliwa walikuwa hawakabi tofauti na ilivyokuwa upande wa Kagere ambaye alikuwa anashuka na kwenda kukaba.

Kwa upande wa ushambuliaji, Chama na Kagere walikuwa wanacheza bila maelewano kiasi ambacho kiliwafanya mabeki wa Ud Songo wacheze kwa kujiamini licha ya kupokea changamoto moja moja walizokuwa wanazipata.

Nahodha wa UD Songo noma

Nahodha wa Ud Songo, Luis Misquissone alionekana kuwa mwiba katika safu ya ulinzi Simba kutokana na namna ambavyo alikuwa na umiliki mzuri wa mpira pamoja na kasi yake.

Luis alikuwa anakaa na mpira kwa muda mrefu hali ambayo iliwafanya mabeki wa Simba kumfanyia madhambi mara kwa mara.

Katika eneo la katikati pia lilionekana kukatika kwa upande wa Simba, hali iliyomfanya Aussems dakika 41 kufanya mabadiliko kwa kumtoa Francis Kahata na kuingia Hassan Dilunga hadi mapumziko kipindi cha kwanza kinamalizika matokeo 1-0.

Katika kipindi cha pili Simba waliingia kwa kasi na kutaka kupata goli lakini mipango yao ilikuwa midogo.

Dakika 57, UD Songo walimtoa Frank Banda na kuingia Cremildo Nhantumbo ili kwenda kuongeza nguvu kwenye eneo la kiungo.

Dakika 62, Simba nao walifanya mabadiliko kwa kumtoa Sharaf Shaboub na nafasi yake ilichukuliwa na Miraj Athuman.

Dakika 64, Pachoio King wa UD Songo, alipewa kadi ya njano baada ya kwenda kumpiga kikumbo kipa Aish Manula.

Dakika 69 UD Songo walifanya mabadiliko kwa kumtoa Stelio Ernesto na kuingia Mario Sinamunda.

Dakika 70 Simba walifanya shambulio kupitia kwa Deo Kanda ambaye alipokea pasi kutokakwa Mkude na kupiga pasi kwa Kanda ambaye alipiga shuti na kipa Charles Swini aliupangua na kuwa kona isiyokuwa na faida.

Simba walionekana kutengeneza nafasi nyingi, lakini umaliziaji ulionekana kuwa tatizo kwa upande wa Simba ambao ulikuwa unaongozwa na Meddie Kagere na Clatous Chama.

Dakika 77 Simba walifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Gadiel Michael na kuingia Mohammed Hussein 'Tshabalala'.

Dakika 79 mpaka 80 Simba waliweza kukaa langoni mwa UD Songo na kulazimisha kupata goli, dakika 80 Deo Kanda alimiliki mpira ndani ya boksi na kupiga shuti ambalo lilidakwa kwa umakini na kipa wa Ud Songo, Charles Swini.

Dakika 83 UD songo walifanya mabadiliko kwa kumtoa Amade Momade na kuingia Mucuapel Tembe.

Dakika 84 Simba ilipata goli kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Erasti Nyoni, baada ya Miraj Athuman kukatwa ndani ya boksi.

Goli hilo liliamsha shangwe za mashabiki waliokuwa wamejitokeza uwanjani, lakini ndoto yao ya kuonda timu yao inasonga mbele ilipotea baada ya filimbi ya mwisho.