Klabu za zaufungukia udhamini mpya Ligi Kuu Bara

Muktasari:

Kupitia mkataba huo, Vodacom Tanzania itatoa fungu la Sh3 bilioni kwa msimu ambayo kwa mujibu wa Rais wa TFF, Wallace Karia, takribani asilimia 75 itagawanywa kwa klabu na 25% ni kwa ajili ya gharama za uendeshaji wa ligi.

KITENDO cha Ligi Kuu Tanzania Bara kupata mdhamini mkuu ambaye ni Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, kimetafsiriwa kama neema na viongozi wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu nchini.
Juzi Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na Vodacom Tanzania walisaini mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Sh9 bilioni kwa ajili ya udhamini wa ligi hiyo ambayo msimu uliopita haikuwa na mdhamini mkuu.
Kupitia mkataba huo, Vodacom Tanzania itatoa fungu la Sh3 bilioni kwa msimu ambayo kwa mujibu wa Rais wa TFF, Wallace Karia, takribani asilimia 75 itagawanywa kwa klabu na 25% ni kwa ajili ya gharama za uendeshaji wa ligi.
“Udhamini huu utahusu maeneo mbalimbali kama vile gharama za uendeshaji, zawadi kwa washindi wa tuzo za mwezi pamoja na washindi wa ligi na pia malipo kwa waamuzi, theluthi mbili ya fedha itakwenda kwa klabu,” alisema Karia.

KLABU KICHEKO KITUPU
Viongozi mbalimbali wa timu za Ligi Kuu, wameutafsiri udhamini huo kama ukombozi kwao wakidai kwa kiasi kikubwa utaleta afueni baada ya kupita katika kipindi kigumu msimu uliopita kutokana na ligi hiyo kutokuwa na mdhamini mkuu.
“Sisi kwanza ni wachanga Ligi Kuu na ukizingatia haikuwa na mdhamini mkuu msimu uliopita, kwetu tunaona ni faraja kubwa kuona Vodacom wametupa udhamini.
Uongozi wa Namungo FC tunatoa pongezi za dhati kwa TFF kwa kazi kubwa waliyofanya hadi kuishawishi kampuni ya Vodacom kukubali kuwa mdhamini Mkuu wa ligi yetu.
Hata kama kiwango cha fedha ambacho klabu tutapata hakitotosha lakini naamini kinaweza kutatua shida zetu kwa zaidi ya asilimia 85 kwani itasaidia kugharamia huduma kama vile chakula, usafiri,matibabu, malazi na hata mishahara. Jukumu lililopo sasa kwetu viongozi wa klabu ni kuhakikisha tunasaka fedha za kukamilisha sehemu itakayobakia,” alisema Mwenyekiti wa Namungo FC, Hassan Zidadu.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa KMC, Walter Harrison alisema,
“Kwanza kabisa ni juhudi ambazo zimezaa matunda na klabu nyingi zilikuwa zinasubiria kwa hamu kwa sababu hazina uwezo mkubwa kiuchumi. Nafahamu inaweza kuibua mijadala juu ya mgawo ambao utaenda kwa klabu maana heri kenda shika kuliko kusingekuwa na mdhamini kabisa. kimsingi mdhamini anatoa fedha ambazo zinalenga kuziwezesha timu zifike vituoni na nadhani msimu uliopita mliona baadhi ya klabu zikikwama mahotelini na kusafiri kwa tabu kwenda vituoni. Lakini pamoja na yote, klabu hazitakiwi kulala. Zinapaswa kuamka na na kutafuta wadhamini ambao watazisaidia kuepuka kutegemea fedha za mdhamini mkuu kumudu gharama zote,” alisema Walter.
Mwenyekiti wa Mbao FC, Solly Njashi alisema msimu uliopita walikuwa na wakati mgumu,hivyo kurudi kwa mdhamini huyo kutapunguza ukali wa maisha kwa timu.
“Kwa jumla ni shukrani kwa shirikisho la soka kwa juhudi za kumpata mdhamini, lakini nishuri zifanyike jitihada pia nyingine kupata mwingine ili kuchochea maendeleo ya mpira,” alisema Njashi.

MWAKYEMBE ATOA NENO
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, ameipongeza Kampuni ya Vodacom kwa kuidhamini Ligi Kuu huku akitoa  wito kwa TFF kuheshimu mkataba huo.
“Niwapongeze Vodacom kwa kuona fursa hii muhimu ya kudhamini ligi yetu. Iko wazi ligi yetu ni moja ya ligi bora duniani kwa sasa. Uendeshaji wa mpira wa miguu ni gharama kubwa sana hivyo kampuni kama Vodacom inapoamua kudhamini, maana yake ina imani kubwa na nyinyi.
“Niwaombe tu TFF kwamba makubaliano mtakayosaini hapa yana masharti yake. Nami naelewa, Vodacom ni kampuni ‘serious’ (makini) kibiashara. Kampuni iliyo makini kibiashara haiwezi kuingia makubaliano na watu wa ajabuajabu. Imeelewa rekodi mpya ya uongozi wa TFF ambao umeonyesha kuwa unaweza kuaminika kwa hiyo nawaomba TFF kwa vile mkataba unakuja na masharti naomba muyazingatie,” alisema Mwakyembe.

VODACOM YAAHIDI MAKUBWA
“Tangu tulipoanza kudhamini Ligi Kuu miaka iliyopita, tumeona hatua kubwa imepigwa kwa soka letu na vijana wengi wameweza kuendeleza vipaji vyao.Udhamini huu ni muendelezo wa juhudi za Vodacom kuendeleza mchezo wa soka hapa Tanzania.
Moja ya mkakati wetu ni kuhakikisha Watazamaji wanaoingia Uwanjani wanapata urahisi wa kununua tiketi kupitia huduma ya Mpesa” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi.

KARIA HUYU HAPA
Rais wa TFF, Wallace Karia, ameelezea mkataba huo kama moja ya ishara za kupanda kwa thamani ya soka la Tanzania, akizitaka klabu kuheshimu mkataba huo huku pia akiahidi neema kwa klabu zilizofanya vizuri msimu uliopita kuwa zitapatiwa zawadi siku chache zijazo.
“Mkataba wetu wa udhamini una masharti yake ambayo tunatakiwa kuyafuata na hatutoruhusu yeyote kwenda kinyume nayo. 
“Masharti hayo ni kama kitabu cha Msahafu na kila mmoja anapaswa kuyafuata. Yeyote ambaye hatoyafuata tutamtoa kwenye familia yetu.
“Ni utaratibu wa kawaida kabla msimu mpya wa ligi haujaanza, washindi mbalimbali wanapatiwa zawadi na niwahakikishie hilo litafanyika ndani ya kipindi cha wiki moja au mbili kutoka sasa.  Kwa bahati nzuri tangu tulipofanya sherehe za kufunga msimu wa 2017/2018 pale Mlimani City na Vodacom, hakukutokea mdhamini mkuu mwingine,” alisema Karia.