Bodaboda za MO kwa wachezaji wa Simba ni kesho tu!

Muktasari:

Mabosi wa Simba wamefichua, zawadi hizo zilizoahidiwa na Mo Dewji kama ahsante kwa wachezaji na benchi la ufundi kwa kutetea ubingwa wa Ligi kuu Bara na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, zitakabidhiwa kesho Jumatatu

NYOTA wa Simba wana kila sababu ya kuanza kutabasamu, kwani mara baada ya mechi yao ya leo dhidi ya UD Songo watakuwa wanahesabu saa tu kabla ya kukabidhiwa zile Bodoboda walizoahidiwa na bilionea wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’ Dewji.
Mabosi wa Simba wamefichua, zawadi hizo zilizoahidiwa na Mo Dewji kama ahsante kwa wachezaji na benchi la ufundi kwa kutetea ubingwa wa Ligi kuu Bara na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, zitakabidhiwa kesho Jumatatu.
Habari za nyota hao wa Simba kupewa bodaboda hizo imekuja wiki mopja na ushei baada ya Mwanaspoti kuanika namna mastaa wa klabu hiyo walivyokuwa gizani bila kujua ni lini watapewa zawadi hizo, huku wengine wakiwa wameshaihama klabu hiyo msimu huu.
Hata hivyo, Mwanaspoti imepenyezewa bodaboda hizo zitakabidhiwa kwa nyota waliokuwepo msimu uliopita ambao wamesalia kikosini Jumatatu ya kesho na zoezi hilo litaendeshwa mubashara ili Watanzania wote waone zoezi hilo.
“Bodaboda zitatolewa Jumatatu eneo la Gerezani na hii imekuja baada ya nyie (Mwanaspoti) kukumbushia, hivyo mkiweza nanyi ruksa kuhudhuria hafla hiyo,” kilisema chanzo cha ndani ya Simba, kilichokataa kutajwa gazetini.
Hata hivyo meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alipotafutwa na kuulizwa juu ya habari hiyo na hasa baada ya mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo (jina tunalo) kutaka atafutwe meneja huyo, alikiri ni kweli Bodaboda zitakabidhiwa Jumatatu.
“Ni kweli Bodaboda hizo zilizoahidiwa na Mwenyekiti wa Bodi wa Wakurugenzi ya Simba, Mo Dewji zitakabidhiwa Jumatatu mapema asubuhi huko huko Gerezani ulikodokezwa,” alisema Rweyemamu alipoulizwa na Mwanaspoti.
Wachezaji Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Emmanuel Okwi, James Kotei, Zana Coulibaly, Do Munishi, Mohammed Ibrahim, Adam Salamba, Haruna Niyonzima na wengine ni kati ya nyota waliokuwa kwenye kikosi cha msimu uliopita ambao wameshasepa timu hiyo.