Mwakyembe awataka TFF walinde mdhamini

Muktasari:

Msimu uliopita wa 2018/2019, Ligi Kuu Tanzania Bara haikuwa na mdhamini mkuu na badala yake ilikuwa na wadhamini washirika ambao ni Kampuni ya Azam Media na Benki ya KCB

Wakati Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likiingia mkataba wa miaka mitatu na kampuni ya Mawasiliano ya Vodacoma kwa udhamini wa Ligi Kuu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amelitaka shirikisho hilo kuheshimu mkataba huo.

Akizungumza katika hafla ya kutangaza udhamini huo, Waziri Mwakyembe alisema namna ambavyo TFF itaheshimu na kulinda udhamini huo utaongeza imani ya Vodacom na kampuni nyingine ya kudhamini mpira wa miguu nchini.

"Uendeshaji wa mpira wa miguu ni gharama kubwa sana hivyo kampuni kama Vodacom inapoamua kudhamini, maana yake ina imani kubwa na nyinyi.

"Niwaombe tu TFF kwamba makubaliano mtakayosaini hapa yana masharti yake. Na mimi naelewa, Vodacom ni kampuni 'serious' (makini) kibiashara. Kampuni iliyo makini kibiashara haiwezi kuingia makubaliano na watu wa ajabuajabu. Imeelewa rekodi mpya ya uongozi wa TFF ambao umeonyesha kuwa unaweza kuaminika kwa hiyo nawaomba TFF kwa vile mkataba unakuja na masharti naomba muyazingatie," alisema Waziri Mwakyembe.

Mkataba huo uliosainiwa jana ni wa miaka mitatu wenye thamani ya Shilingi 9 bilioni