Lampard kuleta mtambo mwingine wa mabao

Muktasari:

Loftus-Cheek kwa sasa anarejea taratibu kutoka kwenye majeruhi, lakini atakapokuwa fiti kwa asilimia 100 atabadilishiwa majukumu ya uwanjani, akitumika tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

LONDON, ENGLAND. MAMBO ni moto huko Stamford Bridge. Kocha Frank Lampard amechungulia mastraika wake wote na kuona kuna shida, hivyo amepanga kuja kivingine kumaliza tatizo la upatikanaji wa mabao.
Kwenye hilo, kiungo huyo wa zamani mwenye hadhi yake huko kwenye kikosi cha The Blues, Lampard ameamua kumbadilishia majukumu ya uwanjani kiungo Ruben Loftus-Cheek ili mambo yaende sawa.
Loftus-Cheek kwa sasa anarejea taratibu kutoka kwenye majeruhi, lakini atakapokuwa fiti kwa asilimia 100 atabadilishiwa majukumu ya uwanjani, akitumika tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
Kwa mujibu wa The Sun, Loftus-Cheek ataanza kutumika kama Namba 9 bandia kwenye kikosi cha Chelsea ili kuleta mabao kutokana na uwezo wa kiungo huyo kwenye kufunga.
Kocha Lampard anataka kumfanya kiungo wake huyo kuongoza safu ya ushambuliaji ili kuifanya timu kuwa na kitu kipya baada ya kuona mastraika wake halisi kumwaangusha kwenye mechi mbili za mwanzo walizocheza kwenye Ligi Kuu England. Tammy Abraham na Olivier Giroud wote wameshindwa kutamba kwenye mechi za kwanza jambo linalowafanya mashabiki kupiga kelele wakimtaka kocha wao kumjaribu Michy Batshuay kuona kama ataweza kufunga na kupata ushindi wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu England. Chelsea watashuka uwanjani kesho Jumamosi kukipiga na Norwich City ugenini kwenye Ligi Kuu England.