Solskjaer amjibu Neville kuhusu penalti ya Pogba

Muktasari:

Lakini, Solskjaer akizungumza kabla ya mechi dhidi ya Crystal Palace itakayopigwa leo Old Trafford, aliwatetea wachezaji wake na kusema kwamba mambo yasikuzwe sana kuhusu mpigaji wa penalti.

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amemjibu Gary Neville anayechonga kuhusu penalti ya Paul Pogba aliyopiga kwenye mechi dhidi ya Wolves na kukosa, akisema kama ni hivyo atateseka kwa sababu kiungo huyo ataendelea sana tu kupigwa mikwaju hiyo.
Kocha Solskjaer alisema Pogba na Marcus Rashford wataendelea kushea majukumu ya kupiga penalti za Man United zinazopatikana na si suala la kulumbana baada ya sare ya 1-1 iliyopatikana dhidi ya Wolves kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uwanjani Molineux Jumatatu iliyopita. Pogba alichukua mpira kupiga penalti hiyo, lakini alikosa baada ya kipa Rui Patricio kuokoa.
Rashford alitaka kupiga penalti hiyo, lakini Pogba alichukua mpira jambo lililotafsiriwa na wengi akiwamo Neville, kwamba Man United hawakuwa wamejipanga juu ya nani apige penalti inapopatikana. Hata hivyo, Neville alionekana kutopenda Pogba kupiga penalti hiyo, aliposema: "Kabla hata hajaenda kupiga penalti ile nilikasirika.
"Rashford alipiga penalti wiki iliyopita, ndiye aliyepaswa kupiga. Timu haikuwa na kiongozi uwanjani, wasingefanya uamuzi ule. Nilikasirishwa na Pogba, kwa sababu ni mbinafsi.Kilikuwa kitu cha kijinga, walipaswa kuamua nani wa kupiga penalti huko kwenye vyumba vyao vya kubadilishia."
Lakini, Solskjaer akizungumza kabla ya mechi dhidi ya Crystal Palace itakayopigwa leo Old Trafford, aliwatetea wachezaji wake na kusema kwamba mambo yasikuzwe sana kuhusu mpigaji wa penalti.
"Hili si jambo ambalo eti tumewaachia wachezaji wenyewe waamue, tuliamua na tuliwachagua wachezaji wawili," alisema Ole na kuongeza. "Sio suala la kuamua na kufanya unavyojisikia. Msimu uliopita tulikuwa na Marcus, Jesse (Lingard), Paul na wote walifunga penalti. Hakuna ugomvi, tumehuzunika hatukushinda mechi.
"Lakini, kuhusu penalti nina uhakika tutaendelea kumwona Paul Pogba akipiga na kufunga penalti zake Man United. Tusubiri tuone itakavyokuwa kwenye penalti nyingine. Tumefanyia mazoezi kupiga penalti na Marcus na Paul wataendelea na majukumu hayo."
Man United itakipiga na Palace uwanjani Old Trafford kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England kesho Jumamosi.