Yajayo Yanga yanafurahisha

HAKUNA asiyejua kwamba klabu ya Yanga katika msimu uliopita ilikuwa ya kuungaunga mno kutokana na kukabiliwa na ukata mkali, lakini msimu huu chini ya uongozi mpya wa Mwenyekiti DK Mshindo Msolla mambo yamekuwa ng'aring'ari na sasa kinachokuja ni balaa na wanayanga wanapaswa kuanza kuchekelea tu.
Hii ni baada ya klabu hii kuanza kuangukiwa na neema baada ya wawekezaji kujitokeza na kuweka biashara zao katika jezi za Yanga.
Mpaka hivi sasa jezi ya Yanga ina wadhamini watatu,Sportpesa (Wazamani), Taifa Gas na Gsm lakini kwa wadhamini hawa wapya kumekuwa na uficho mkubwa juu ya mkataba waliosaini pamoja na pesa zilizowekwa mezani.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amefichua klabu yao kwa sasa ipo na mipango mingi ya kujaza wadhamini na baadhi wameanza kujitokeza hadharani na hiyo ni neema kwa klabu hiyo.
Mwakalebela alisema mpaka wadhamini hao wanakaa katika jezi zao, inamaanisha kwamba tayari wameshaafikiana kila kitu baina ya pande mbili.
"Siwezi kusema moja kwa moja kwamba tumesaini mkataba wa miaka mingapi na tumepata kiasi gani hivi sasa, lakini ifahamike kwamba mpaka wanakaa katika jezi zetu basi tayari tumeshaafikiana kwa asilimia 100, lakini tutaweka kila kitu wazi na watanzania watajua," alisema.
Aliongeza kwa upande wa jezi wameweka kipengele cha kuchukua 1300 katika kila jezi ambayo itakuwa inauzwa na kampuni ya GSM.
Akizungumzia upande wa wadhamini wengine wanaotaka kudhamini klabu hiyo, alisema "Tupo katika mazungumzo na baadhi ya kampuni kutoka upande wa waandaji wa chakula lakini pia na kampuni moja ya simu, mambo yote yakiwa tayari tutatangaza," alisema.
Juzi kati GSM ilifichua kuingia mkataba wa mwaka mmoja na Yanga kwa ajili ya bidhaa zao za Magodoro, nembo itakayokaa mgongoni juu ya namba ya mchezaji ikiwa kama ni jibu la wapinzani wao Simba wanaovaa jezi yenye nembo ya Mo Halisi ya bilionea wao, Mohammed Dewji.