Mshambuliaji wa Ghana, Junior Agogo afariki dunia

Muktasari:

Agogo amecheza katika klabu za Queens Park Rangers, Nottingham Forest, Sheffield Wednesday, Bristol Rovers huku Afrika akiichezea Zamalek ya Misri.

Dar es Salaam. Aliyekuwa mshambuliaji wa Ghana na Queens Park Ranger, Junior Agogo amefariki leo baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Agogo amefariki katika hospitali ya London nchini England alikokuwa akipatiwa matibabu.

Tangu mwaka 2015 Agogo afya yake iliyumba akisumbuliwa na kiharusi hatua ambayo ilizalishwa baada ya kufilisika kufuatia kutalikiana na mkewe kisha asilimia kubwa ya mali zake ikichukuliwa na mkewe.

Kuugua kwake kulimfanya kwa muda mrefu asionekane hadharani na kuwa mtu aliyeadimika mpaka sasa umauti unamkuta huku pia ikilelezwa hali hiyo ilimuumiza zaidi baada ya wachezaji wenzake wa Black Stars kutokuwa karibu naye katika kipindi hicho kugumu hali iliyomuongezea msongo wa mawazo.

Mkapa anafariki Agogo maisha yake yalikuwa na mabadiliko makubwa ikilezwa alikuwa anaishi katika nyumba ndogo isiyokuwa na hadhi yake akisaidiwa na mama yake mzazi na mbwa wake.

Agogo amefanikiwa kuichezea Ghana jumla ya mechi 27 na kufunga jumla ya mabao 12.

Agogo aliyezaliwa miaka 40 iliyopita klabu yake ya mwisho kuitumikia ni Hibernian ya Scotland, lakini amewahi kuitumikia klabu mbalimbali  za England zikiwemo baadhi zikiwa Queens Park Rangers, Nottingham Forest, Sheffield Wednesday, Bristol Rovers huku Afrika akiichezea Zamalek ya Misri.