Dk Msolla aisuka upya kamati ya sheria, nidhamu Yanga

Muktasari:

Mapande ameendelea kuhudumu vyombo vya sheria ndani ya Yanga baada ya awali kuwa katika kamati ya uchaguzi na sasa anahamishiwa kamati ya Sheria na nidhamu.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla ameunda kamati ya watu tisa watakaoongoza kamati ya sheria na nidhamu ya klabu hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa leo Msolla amempa jukumu la kuongoza kamati hiyo mwanasheria mkongwe Sam Mapande ambaye ameendelea kudumu katika kamati za sheria ndani ya klabu hiyo.

Awali Mapande alikuwa katika kamati ya uchaguzi ya Yanga ambayo ilishirikiana na kamati ya uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwenye mchakato wa uchaguzi uliouingiza uongozi wa Msolla Madarakani.

Mbali na Mapande wajumbe wengine nane katika kamati hiyo ni pamoja na Esther Cheyo, Sharif Makosa, Shaban Mgonja.

Wajumbe wengine ni Benjamin Mwakasonda aliyekuwa mmoja wa wagombe ujumbe katika nafasi ya ujumbe wa klabu hiyo kwenye uchaguzi uliopita, Phillipo Bura, Seleman Jongo, Marry Mavula na Cosmas Chidumule.