Jicho la Mwewe: Salamba anaweza kuwa Wilfried Zaha

Monday August 19 2019

Jicho la Mwewe, Mwanaspoti, Tanzania, Salamba anaweza, kuwa Wilfried Zaha

 

By Edo Kumwembe

JINSI kasi ya maisha ilivyo. Nilimuuliza kocha wa wakati huo wa Lipuli, Suleiman Matola wakati Simba ilipokuwa wanahaha kumnasa mshambuliaji wake, Adam Salamba. Nilimuuliza kuhusu ubora wa Salamba.
Akaniamba Simba walikuwa wamempata mchezaji ambaye akipewa nafasi vizuri akaaminiwa basi watamsahau Emannuel Okwi. Nilicheka. Nilipata hamu ya kumuona Salamba. Hata Simba wenyewe walikuwa na hamu naye kiasi kwamba alikuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa Msimbazi dirisha la mwaka 2017.
Akapewa pesa ndefu, akanunua gari aina ya Mark X, akapata nalo ajali. Ndani ya uwanja maisha yake yakawa pia ya ‘kiajaliajali’. Leo ametua katika klabu ya Namungo FC. Klabu iliyopo wilaya fulani mbali kutoka Lindi Mjini. Sio tena yule ‘Emmanuel Okwi’ ambaye alianiambia Matola.
Wachezaji kama kina Salamba wamekuja wengi na wameondoka. Kitu gani Simba ilikiona kwa Salamba mpaka ikamkimbilia vile? Lazima ni mchezaji ambaye ana kitu. Lazima. Sio bure kwamba ilimsajili kwa haraka haraka vile ili Yanga na Azam zisimuwahi.
Kimekwenda wapi kitu walichokiona? Hapa ndipo tunapokwama. Inawezekana kuna mambo matatu. Kwanza kabisa, inawezekana mchezaji mwenyewe hakuwa tayari kucheza katika timu kubwa. Ukitoka timu ndogo kwenda timu kubwa unahitaji maandalizi ya kiakili.
Ukitoka timu ndogo inamaanisha ulikuwa samaki mkubwa katika kundi la samaki wengi ndani ya bwawa dogo. Ukienda timu kubwa unakuwa samaki wa kawaida ndani ya samaki wengi wakubwa katika bwawa kubwa.
Unahitaji kupambana kuliweka jina lako juu. Inanikumbusha jinsi ambavyo Mbwana Samatta alitua Simba akitokea African Lyon. Akakuta majina makubwa ya Mussa Hassan ‘Mgosi’ na  Okwi. Hata hivyo, akapenya na kuwa staa kisha akaondoka zake.
Salamba amekutana na kizingiti cha Meddie Kagere na John Bocco ameshindwa kupenya. Inawezekana kwa sababu kiakili alikuwa anajiandaa vilevile kama alivyokuwa anajiandaa Lipuli. Inawezekana hakuibadili akili yake.
Inawezekana aliendelea kuwa na mambo mengi nje ya uwanja wakati Bocco na Kagere wanajulikana kwa kutokuwa na mambo mengi nje ya uwanja. Simba na Yanga zilipokea wachezaji wengi wa aina hii na wakajisahau kwamba wamekwenda katika timu kubwa. Wakaishi kama wapo Ujenzi Rukwa au Milambo ya Tabora.
Kitu kingine ambacho huenda kimemtokea Salamba ni kushuka kwake kujiamini. Mashabiki hawakumtengenezea kujiamini. Benchi la ufundi halikumtengenezea kujiamini. Na kama moyo wake ni laini basi anguko lake lilikuwa linatazamiwa.
Anaposajiliwa mchezaji kama Kagere baada ya wewe, macho ya mashabiki yanakwenda kwa Kagere kwa sababu ametokea nje ya nchi na amenunuliwa na pesa ndefu. Anapokosea Kagere mashabiki wanapiga makofi. Anapokosea Salamba mashabiki wanazomea. Ghafla anatokea shabiki mmoja anasimama mbele ya jukwaa na kudai ‘Salamba ana jimama pale Magomeni ndio linamuharibu’. Haya ni maisha ya kawaida ya mashabiki katika mchakato wa kushusha uwezo wa kujiamini kwa mchezaji.
Baadaye mchezaji anakuwa anauogopa mpira. Anakuwa tofauti na Salamba aliyekuwa anausaka mpira kila dakika pale Lipuli. Kuna wachezaji wachache wa Kitanzania waliweza kuhimili vishindo vya kucheza na mastaa wa nje. Mmojawapo alikuwa Simon Msuva.
Wakati akianza Yanga, Msuva alikuwa amezungukwa na mastaa. Akili yake ilikuwa haijakaa sawa na kila mara alikuwa anazomewa na mashabiki wa Yanga. Baadaye akili yake ilikaa sawa na akaibuka kuwa shujaa pale Yanga. Alikuwa staa mkubwa pengine kuliko wachezaji wa kigeni waliokuwa wanalipwa pesa nyingi zaidi yake.
Tatizo jingine la Salamba ni lile la kila siku. Tatizo linalosababishwa na makocha wetu na watu wa benchi la ufundi. Wachezaji wetu hawaimarishwi. Wanacheza vilevile siku zote. Kila mchezaji anacheza kama anavyocheza kwa miaka yetu. Mapungufu yake yanakuwa yaleyale.
Katika umri wake, Salamba alipaswa kuimarishwa katika mapungufu yake ili aweze kufika katika anga za kina Kagere. Lakini aliendelea kuwa yuleyule. Sidhani kama watu wetu wa benchi la ufundi wana muda wa kushughulika na mchezaji mmoja mmoja.
Pamoja na yote haya nadhani mchezaji kama Salamba anaweza kurudi tena timu kubwa kama akituliza kichwa chake. Kama kuna kitu Simba walikiona kutoka kwake, basi bado kipo na bado amezaliwa nacho. Kilichomtokea kiliwahi kuwatokea wachezaji wengi nchini.
Hassan Dilunga alionekana kuchemsha Yanga lakini alipoenda klabu nyingine za katikati ya msimamo wa ligi alituliza kichwa akaanza kutamba. Hatimaye amerudi Simba na ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo.
Iliwahi pia kumtokea Ustaadhi Amri Kiemba. Aliwahi kupotezwa na Yanga akaenda timu za kawaida. Akatuliza kichwa na kucheza soka la uhakika kabla hajaibukia Simba na kuwa mchezaji tegemeo klabuni. Siamini kama kuna mchezaji wa timu ndogo na timu kubwa. Naamini katika kuimarika kiakili kwa mchezaji.
Wilfried Zaha ni mchezaji mwingine ambaye aliwahi kununuliwa na timu kubwa, Manchester United, akitokea Crystal Palace, akachemsha, akarudi Palace, lakini sasa ameonyesha uwezo mkubwa na klabu kubwa zinamtaka tena.

Advertisement