Aishi Manula aukubali mziki wa Kakolanya

Muktasari:

Manula aliyekuwa jukwaani juzi Jumamosi akimshuhudia, Kakolanya akiokoa michomo ya washambuliaji wa Azam FC kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii na timu hiyo kuondoka na ushindi wa mabao 4-2

Dar es Salaam. MWENYEWE kakubali. Kipa namba wa Simba, Aishi Manula aliye majeruhi kwa sasa amekiri uwepo wa Benno Kakolanya kwenye kikosi hicho kuna maana kubwa hasa katika kuisaidia timu hiyo kufikia malengo yao ndani ya msimu huu.
Manula aliyekuwa jukwaani juzi Jumamosi akimshuhudia, Kakolanya akiokoa michomo ya washambuliaji wa Azam FC kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii na timu hiyo kuondoka na ushindi wa mabao 4-2.
“Kwangu Kakolanya siku zote ni kipa mzuri na ninapomwona naona anafanya vizurisina shaka, kwani Simba ilimsajili Kakolanya ili aje kuisadia kufikia mafanikio, tukiwa pamoja, Kakolanya au Ally Salim wote tunashirikiana ili kufikisha timu pale inapotaka kufika,” alisema Manula.
Aliongeza kikosi cha timu ni kikosi bora zaidi kwa maana kinacheza kwa umakini japo kuna makosa madogomadogo yanayofanywa ambayo kimchezo siku zote hayawezi kukwepeka kwenye timu, japo wanajitahidi kufanya kile ambacho kila mmoja anafurahishwa nacho.
Tangu Simba irejee nchini kutoka Afrika Kusini ilipoweka kambi, Manula hajaonekana langoni kutokana na kutokuwa fiti na kusababishwa kuondolewa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichokuwa kinajiandaa na mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki Chan mwaka ujao ilipocheza na dhidi ya Kenya.
Siyo Manula pekee aliyeonekana jukwaani juzi, hata wachezaji wa Azam FC kama vile Aggrey Morris, Idd Seleman ‘Nado’, Daniel Ngoma pamoja na Daniel Amoah nao waliushuhudia mchezo huo wa Ngao ya Jamii wakiwa kama mashabiki  huku Azam ikilala 4-2.