PSG, Neymar na kisa cha sizitaki mbichi hizi

Muktasari:

Mabingwa hao wa Ufaransa wanataka kulipwa Pauni 200 milioni kwenye mauzo ya mchezaji huyo, huku Barcelona wakidaiwa kuwa mstari wa mbele kwenye mazungumzo ya mshambuliaji huyo wa Kibrazili.

PARIS, UFARANSA. PARIS Saint-Germain wamegoma kufuta kabisa uwezekano wa supastaa wao Neymar kubaki na kuendelea kukipiga kwenye kikosi chao msimu huu.
Neymar amekuwa akihusishwa na mpango wa kuihama timu hiyo huku wababe wa La Liga, Real Madrid na Barcelona wakiripotiwa kufukuzia saini yake kabla ya dirisha hili la majira ya kiangazi kufungwa.
Lakini, siku zinakwenda kasi kwelikweli jambo ambalo linawafanya PSG kuwa na mawazo ya kwamba kama staa wao huyo hajahama, basi watakuwa tayari kufanya naye kazi bila ya kujali yanayoendelea kwa sasa.
Mabingwa hao wa Ufaransa wanataka kulipwa Pauni 200 milioni kwenye mauzo ya mchezaji huyo, huku Barcelona wakidaiwa kuwa mstari wa mbele kwenye mazungumzo ya mshambuliaji huyo wa Kibrazili.
Barca walijaribu kutoa ofa ya wachezaji ili kupunguza ukubwa wa bei hiyo, lakini sasa mmoja wa wachezaji iliyokuwa ikiwaweka kwenye ofa, Philippe Coutinho ametimkia zake kwa mkopo Bayern Munich. Marca linaripoti kwamba PSG bado wana matumaini makubwa ya kubaki na Neymar kwenye kikosi chao licha ya kwamba uhusiano wa mchezaji huyo na mabosi wake umekuwa kwenye mashaka makubwa.
Neymar hakujumuishwa kwenye kikosi cha PSG kilichocheza na Rennes kwenye Ligue 1 jana Jumapili, lakini kocha Thomas Tuchel hiyo ni kwa sababu tu mchezaji huyo bado hajapona vyema majeruhi yake na si suala la kuhama.