Samatta aweka rekodi mpya ya mabao KRC Genk

Muktasari:

Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta anaifukuzia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa KRC Genk ya Ubelgiji.

Dar es Salaam. Baada ya kufunga mabao matatu mshambuliaji Mbwana Samatta ‘Samagoal’ amefikisha mabao 70 na kuivunja rekodi ya Kevin Vandenbergh aliyefunga mabao 68 katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa KRC Genk.

Samatta jana alifunga mabao matatu na kuiongoza Genk kuichapa Waasland-Beveren kwa magoli 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Ubelgiji.

Mabao hayo matatu yanamfanya nahodha wa Tanzania kushika nafasi ya tatu kwa mfungaji bora wa muda wote wa KRC Genk kwa muda mfupi tangu ajiunga na timu hiyo akitokea TP Mazembe mwaka 2016.

Kabla ya Samatta kufikisha rekodi ya mabao 70, Genk aliyekuwa akishikiria rekodi hiyo alikuwa Vandenbergh aliyefunga mabao 68 ambaye kwa sasa anaichezea SC Aarschot.

Anayeongoza katika rekodi hiyo ya wafungaji bora wa muda wote wa KRC Genk ni Jelle Vossen aliyeifunga mabao 105 huku nafasi ya pili akiwa, Wesley Sonck mwenye mabao 80.

Samatta ananafasi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa KRC Genk kama ataendelea na kasi aliyonayo kwenye ufungaji hasa ukizingatia Sonck ametundika daruga  huku  Vossen akimalizia soka lake Club Brugge KV.

Hat trick aliyofunga Samatta kwenye mchezo walioshinda mabao 4-0, imemfanya afikishe mabao manne msimu huu kwenye Ligi, ambayo pia yanamfanya awe sawa kwa mabao na Dieumerci Mbokani wa Royal Antwerp na Okereke wa Club Brugge.

Msimu uliopita Samatta aliifungia KRC Genk mabao 23 kwenye Jupiler Pro, yaliyoisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa.

Katika vita ya msimu uliopita ya kuwania ufungaji bora Samatta alizidiwa mabao mawili na Harbaoui ambaye alifunga  mabao 25 huku kwenye idadi hiyo akibebwa na penalti nyingi alizokuwa akipiga.

KRC Genk kabla ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya Waasland-Beveren, walipokea vipigo viwili mfululizo kutoka kwa Mechelen cha mabao 3-1 na kingine kilitoka kwa Zulte-Waregem cha mabao 2-0.