Tanzania yaondoshwa Michezo ya Afrika kabla ya ufunguzi

Muktasari:

Tanzania inashiriki michezo hiyo ikiwa na historia ya kufanya vizuri tangu 1965 iliposhiriki mara ya kwanza hadi 2011 na mwaka 2015 kwa mara ya kwanza ilitoka kapa kwenye michezo iliyofanyika Congo Brazzaville huku msimu huu ikishiriki mara ya 12.

Dar es Salaam. Licha ya hafla ya ufunguzi wa michezo ya Afrika (All African Games) kufanyika kesho Jumatatu mjini Rabat Morocco, tayari timu judo ya Tanzania imeondoshwa katika michezo hiyo.

Wachezaji judo wa Tanzania, Abdulrabi Alawi, Anangisye Pwele na Khamis Hussein watapeperusha bendera ya Tanzania katika hafla ya ufunguzi kesho Jumatatu wakiwa tayari wameondolewa mashindanoni.

Wachezaji hao wamepigwa katika michezo yao ya kwanza ya mtoano hatua ya 32 bora juzi Jumamosi, na kuondolewa mashindanoni.

Alawi alichapwa na Herikanto Andriamanoelina wa Madagascar katika uzani wa kilogramu 66, Pwele aliyechezea kilogramu 73 alipigwa na Ayton Siquir wa Msumbiji na Ali aliyechezea kilogramu 81 alipigwa na Mohamed Ahmed wa Sudan.

Nafasi pekee ya Tanzania katika michezo hiyo imesalia kwenye riadha ambao bado hawajaondoka nchini, hivyo hawatokuwepo katika hafla ya ufunguzi leo itakayoongozwa na mfalme wa Morocco, Mohammed VI kwenye Uwanja wa Complexe Sportif Prince Moulay Abdellah.

Msafara wa riadha wenye wa wachezaji sita na kocha Mwinga Mwanjala, utaondoka nchini keshokutwa Jumanne kuelekea Morocco katika michezo hiyo ambayo kwa mujibu wa Makamu wa pili wa Rais Ufundi wa RT, Dk Hamad Ndee wamelazimka kuchelewa kutokana na michezo yao kule kuchelewa kuanza.

"Timu itaondoka Agosti 20 na mashindano yao Morocco yataanza Agosti 23 na watarejea Septemba Mosi," alisema Dk Ndee.