Tshishimbi: Angekuwepo Makambo Yanga ingetisha zaidi

Muktasari:

Yanga ipo jijini Arusha leo inatarajia kushuka uwanjani kumenyana na AFC Leopards ukiwa ni mchezo wa kirafiki kujiandaa na mchezo wa marudiano ligi ya Mabingwa dhidi ya Township Rollers Agosti 24.

Dar es Salaam. Nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi amesema mshambuliaji Heritier Makambo alihitajika zaidi msimu huu kutokana na uzoefu wake wa Ligi Kuu Bara aliokuwa nao.

Makambo ameondoka Yanga akiwa ni mfungaji bora wa klabu hiyo baada ya kuifungia mabao 18 akiwa amecheza msimu mmoja na kutimkia Horoya ya Guinea.

Tshishimbi alisema usajili uliofanya msimu huu ni bora, lakini tatizo linakuja nyota wengi ni wageni wa ligi hiyo hasa safu ya ushambuliaji itakuwa changamoto kwao, lakini angekuwepo Makambo basi Yanga isingekamatika.

"Kumkumbuka Makambo haina maana usajili uliofanywa unamakosa hapana nimemkumbuka kwa sababu tayari alikuwa ameshazoea mazingira na kutengeneza safu iliyokuwa inaelewana zaidi hivyo angeendelea kuwepo angekuwa chachu ya ushindi katika timu," alisema na kuongeza kuwa.

"Mwanzo ni mgumu hata Makambo alianza vibaya, lakini baadaye alikuwa bora kwa upande wa nyota wa sasa wanakuwa na wakati mgumu zaidi kwani timu ipo katika mashindano ambayo yanahitaji mabao zaidi na pointi ili kuweza kusonga hatua nyingine tofauti na kipindi cha Makambo," alisema Tshishimbi.