Mashemela Gor Mahia, Ingwe wakusanya mbogi

Muktasari:

Usajili wake unamfanya kuwa mchezaji wa 18 kusainiwa na Gor kabla ya msimu mpya kuanza. Huenda akawa sajili wa mwisho atakayetegemewa sana kuimarisha safu ya mashambulizi

MABINGWA watetezi Gor Mahia na mashemela wao, ukipenda mashemeji, AFC Leopards, wameendelea kufanya usajili mkubwa licha ya kuwepo na hofu kuwa huenda msimu mpya wa ligi utasita kuanza jinsi ilivyoratibiwa.
Hivi majuzi Gor ilidhibitisha kumwongeza wing’a Clifton Miheso kwenye mbogi yao ya wachezaji 18 wapya iliyowasajili hadi kufikia sasa.
“Gor Mahia imemsajili wing’a wa kimataifa Clifton Miheso kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kumfurahisha Kocha Steven Pollack kwenye mechi ya CHAN 2020 dhidi ya Tanzania na ya kirafiki dhidi ya Gor alipokuwa na Police FC ya daraja la pili” taarifa ya Gor ilieleza.
Usajili wake unamfanya kuwa mchezaji wa 18 kusainiwa na Gor kabla ya msimu mpya kuanza. Huenda akawa sajili wa mwisho atakayetegemewa sana kuimarisha safu ya mashambulizi. Gor Mahia imefanya usajili huo mkubwa baada ya kuwapoteza takriban wachezaji saba wa kikosi chake cha kwanza cha msimu uliopita kuanzia kiungo mbunifu Francis Kahata, wing’a George Odhiambo, straika Jacques Tuyisenge, Francis Mustapha, Erisa Ssekisambu na nahodha Haroun Shakava nakipa Shaban Odhoji,
Kwa wakati huo, nao watani wao wa tangu jadi, mashemela Ingwe nao wamefikisha idadi ya mbogi ya usajili wao kuwa 10, baada ya kuwoangeza wengine watatu.
Watatu hao ni beki wa kulia, Collins Shivachi kutika Tusker, pamoja na viungo, John Wanda na Collins Shichenje. Tayari Ingwe ilishawaachia huru wachezaji wanane.
Usajili huu mkubwa umeendelea licha ya bodi inayoendesha Ligi Kuu nchini KPL kusema kuwa haina uhakika wa ligi kuanza Agosti 31 jinsi ilivyoratibiwa baada ya Mdhamini Mkuu Sportpesa kujichuja.