Wanyama ahesabu magethaa tu

Muktasari:

Tangu msimu uliopita ulipomalizika, ripoti kibao zimemuhusisha na kujiunga na klabu mbalimbali. Hata hivyo, duru zinaarifu kuna uwezekano mkubwa akaishia zake Uturuki kabla ya dirisha la usajili kufungwa rasmi mwisho wa mwezi ujao.

TETESI za nahodha wa Harambee Stars Victor Wanyama kuihama Tottenham Hotspurs zimekolea huku ripoti za sasa zikiarifu kiungo huyo anahesabu magethaa tu kabla ya kuishia zake Uturuki.
Tangu msimu uliopita ulipomalizika, ripoti kibao zimemuhusisha na kujiunga na klabu mbalimbali. Hata hivyo, duru zinaarifu kuna uwezekano mkubwa akaishia zake Uturuki kabla ya dirisha la usajili kufungwa rasmi mwisho wa mwezi ujao.
Wanyama mwenyewe hivi majuzi alidokeza kuwa muda wake uwanjani White Hart Lane huenda umefikia kikomo baada ya kuposti picha ya jezi lake alilovalia kwenye fainali ya Champions League na kuambatanisha na maelezo ‘Sijui kama pengine huu ndio muda mwafaka wa mimi kuaga”.
Na sasa kwa mujibu wa ripoti kutoka Uturuki ni kwamba, miamba wa ligi ya taifa hilo, Fenerbeche ilikuwa imemuulizia ila kwa mkopo. Pili ilitaka kama ikimchukua kwa mkopo, ilipe asilimia 60% ya mshahara anaoupata kwa kipindi itakachokuwa naye huku klabu yake ikitakiwa kujaliza.
Hata hivyo, ofa yao inaripotiwa kusukumwa pembeni baada ya wapinzani wao miamba Galatasary kujiongeza huku ofa yao ikiwa ni ya kumsaini mazima. Tayari Galatasaray inasemekana kutuma ujumbe wake mjini London ukiongozwa na Sukru Haznedar kwenda kusukuma dili hiyo. Imani ya Kocha Mauricio Pochettino kwa Wanyama imedidimia sana kutokana na majeruhi ya mara kwa mara ambayo yamemkumba Wanyama baada ya kutamba kwenye msimu wake wa kwanza.  Msimu uliopita, Wanyama ambaye angali na miaka miwili kwenye mkataba wake, alitumika mara nne tu kwenye mechi za ligi kutokana na majeraha ya kujirudia.
Na japo wikendi iliyopita alianza benchi dhidi ya Aston Villa, msimu huu kama akiamua kubakia Hartlane huenda ukawa mgumu hata zaidi baada ya Spurs kuwasajili viungo wawili Tanguy Ndombele na Giovanni Lo Celso.