Migne: FKF manzee tusisumbuane

Muktasari:

FKF iliamua kumtimua kazi Migne mapema wiki hii huku kwenye taarifa yake ikisema pande zote zilikuwa zimeafikiana kuvunja mkataba wake baada ya kujadiliana namna ambavyo kocha huyo atalipwa fidia yake.

MFARANSA Sebastian Migne aliyefutwa kama Kocha Mkuu wa Harambee Stars ameondoka na machungu akiionya shirikisho la soka nchini FKF kuhakikisha linatimiza ahadi ya kumlipa fidia yake kwa mujibu wa makubaliano lau sivyo itakula kwao.
Kocha huyo ameiambia FKF kuwa hawapaswi kusumbuana kabisa kwenye suala la malipo yake ya fidia lau sivyo watavutana.
FKF iliamua kumtimua kazi Migne mapema wiki hii huku kwenye taarifa yake ikisema pande zote zilikuwa zimeafikiana kuvunja mkataba wake baada ya kujadiliana namna ambavyo kocha huyo atalipwa fidia yake.
Migne alikuwa akilipokea mshahara wa Sh1.5 milioni kila mwezi na mkataba wake na Stars ulikuwa angali una miaka miwili zaidi.
Hata hivyo, baada yake kuzalisha matokeo duni katika dimba la AFCON kisha kubanduliwa nje ya Kombe la CHAN 2020 na Tanzania, presha ya kumtimua ikaibuka. Awali FKF ilisita kwa kuhofia gharama kubwa ambayo ingeandama uamuzi huo.
Hata hivyo,  baada ya presha kuzidi hasa kutoka kwa watu wenye ushawishi mkubwa katika soka la Kenya na pia wanasiasa, FKF ilikosa namna na kumtimua.
Sasa kocha huyo mjeuri aliyekuwa ametishia FKF kudhubutu kumtimua ameondoka na vijembe vyake akitishia kuitesa FKF endapo itashindwa kutimiza ahadi yake ya kumlipa fidia yake kwa mujibu wa makubaliano.
“Sina wasiwasi na kulipwa fidia yangu kwa sasa kuna utaratibu mwingi wa kufuatwa kama ikitokea wagande. Kuna FIFA na pia zipo njia nyinginezo ambazo zinaweza kufuatwa ila sifikiri kama tutafikia hapo,” Mgine katishia.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita FKF tayari imeshapoteza kesi mbili dhidi yao baada ya kuwavunjia mikataba makocha wawili kabla ya muda.
Mahakama ya kimichezo yenye makao yake kule Lausanne, Swirtzerland CAS, iliiamrisha FKF kumlipa marehemu Kocha Mfaransa Henri Michel Sh4.5 milioni na Kocha Mbelgiji Adel Amrouche Sh60 milioni wote ambao mikataba yao ilikiukwa.