Mbeya City yampa akili Katwila

Muktasari:

Katwila amefafanua kuwa ametengeneza mfumo wa wachezaji ambao ataona wanafaa kucheza mechi za nyumbani na ugenini na kuhakikisha wanapata matokeo.

ZIKIWA zimebakia siku sita kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila amesema katika kikosi chake hatakuwepo mchezaji wa kudumu na namba na kwamba mechi yao ya Mbeya City imewapa akili ya kujua wapi kuna tatizo.
Mtibwa ilicheza mechi ya kirafiki na Mbeya City, Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro na kupigwa bao 1-0 na Katwila alisema kipigo hciho hakijamsumbuam, bali kimemsaidia kujua wanakwama wapi mapema.
"Ligi tunaanza na Lipuli ya Iringa ambao sisi tutawafuata, naamini tupo vizuri kwa ajili ya kuanza msimu na mafanikio ingawa nikiri tunawaheshimu wapinzani wetu," amesema.
Katwila amefafanua kuwa ametengeneza mfumo wa wachezaji ambao ataona wanafaa kucheza mechi za nyumbani na ugenini na kuhakikisha wanapata matokeo.
Amesema hana kawaida ya kuwa na kikosi cha kwanza, akidai wachezaji ambao wamesajiliwa wanatakiwa kufanya kazi kwa kushindana na sio baadhi kutumika sana.
"Huwa naandaa kikosi chote, sina wachezaji wa kikosi cha kwanza, ninachofanya naangalia aina ya mechi nani acheze na nani asicheze, pia ambao watacheza nyumbani na ugenini.
"Maandalizi yamekamilika kama kesho Jumapili tutafanikiwa kucheza mojawapo na timu kati ya Polisi Dodoma ama Polisi Kombaini basi itakuwa mechi ya mwisho," amesema.