Sababu za FKF kuchujwa Migne Harambee Stars hizi hapa

SIKU 11 zilizopita baada ya Harambee Stars kubanduliwa nje ya dimba la CHAN 2020 na Tanzania, kocha Sebastian Migne alipoulizwa kama atajiuzulu wadhifa wake kutokana na matokeo duni aliyozalisha, alitishia Shirikisho la Soka nchini (FKF), kutothubutu.

Mawazo yake yalikuwa ni kwamba kumfuta kazi itaikosti FKF kwani ana mkataba na pia chombo hicho kimekuwa kikishindwa kumlipa inavyotakiwa hivyo kumchuja itakuwa hata vigumu zaidi kumfidia.

“Kama shirikisho linataka kunifuta basi wanifute. Ila kama kunilipa mshahara wangu ni tatizo, wataweza kunifidia mkataba wangu wakiuvunja,” alijibu kwa ujeuri.

Hata hivyo, kama wasemavyo Wahenga “kuwa makini na unachooomba.” Jumanne ya wiki hii FKF ilimfuta kazi huku kwenye taarifa yake ikisema ilikuwa imefikia makubaliano na Migne kuvunja mktaba wake na pia kuelewana jinsi itakavyomlipa fidia yake. 

FKF ilimtupia Migne virago vyake nje licha ya hapo awali kusisitiza kwamba haikuwa na mawazo hayo, licha ya matokeo duni aliyozalisha ikishikilia kuwa uamuzi huo utaigharimu takriban Sh50 milioni za kumlipa kama fidia. FKF ilisisitiza  kuwa kwa sasa imesota kinoma hivyo haina jinsi ila kumvumilia tu na Mfaransa huyo.

Hata hivyo, duru zinaarifu kwamba presha kubwa kutoka kwa wadau mbalimbali wenye ushawishi wakiwemo wanasiasa na maafisa serikalini ndio uliochochea Migne kuachishwa kazi.

Kushindwa kutamba kule AFCON kidogo ilieleweka ikizingatiwa kwamba Stars walikuwa wakirejea katika dimba hilo baada ya kuwa nje kwa miaka 15. Hata hivyo kuchujwa kwa Stars kwenye CHAN tena na timu ya kiwango cha Tanzania ndicho kilichowachefua zaidi wadau na kumzidishia presha Mwenyekiti wa FKF, Nick Mwendwa ambaye kwa kukosa jinsi akafanya kama walivyotaka. Hangeweza tena kumtetea Migne.

Lakini kando na presha hizo, kilichovuruga zaidi urojo wake Migne ni kwamba alikuwa kapitana na baadhi ya wachezaji katika kikosi cha taifa hivyo uhusiano wake mbaya nao haungeruhusu yeye kuendelea.

Afisa mmoja wa kutoka AK alituarifu kuwa, “tulikuwa tushamchoka jamaa, kashindwa kabisa kuzalisha matokeo wakati mashahara tunaompa ni mkubwa. Kufutwa kwake ingetokea tu haingeupukika.”

Kocha huyo alizua utata hata zaidi kutokana na timu aliyoiteua kwenda nayo AFCON akiwaacha wachezaji kadhaa waliokuwa kwenye fomu nzuri jambo ambalo liliwaudhi wengi.

Migne kaondoka baada ya kuwa mamlakani kwa miezi 14.

Anakuwa kocha wa tatu kuchujwa Stars toka 2016 Mwenda alipochukua usukani wa shirikisho. Watangulizi wake ni Stanley Okumbi na Mbelgiji Paul Put aliyedumu kwa miezi mitatu tu.