Wazito wa wazito FC kuchachisha mwendo wa Manchester City

USAJILI walioufanya na Wazito FC tayari kwa msimu huu mpya wa KPL unaweza kusema ni sawa na ule ulioshuhudiwa pale Man City katika kipindi cha misimu iliyopita.

Yaani Wazito FC wamewavuta wazito tupu katika harakati zao za kuunda kikosi dhabiti.

Wazito FC inamilikiwa na tajiri mmoja mzungu kwa jina Ricardo Badoer aliyeinunua Disemba ya 2018 ikiwa inashiriki Ligi ya Divisheni ya Pili – National Super League (NSL).

Tangu kipindi hicho kamwaga  mamilioni ya kutosha kuiboresha timu hiyo ikiwemo kununua basi la timu kwa gharama ya Sh12 milioni.

Lakini baada ya Wazito kufanikiwa kupanda daraja hadi Ligi Kuu ya KPL msimu huu baada ya kuibuka mabingwa wa NSL 2017/18, milionea huyo kamwaga mkwanja zaidi wa zaidi ya Sh8 milioni kufanya usajili mpya.

Tayari Wazito wamewasaini wachezaji 11 ambao wote ni wazito wa KPL kutokana na uzoefu walionao katika ligi hiyo.

Mmoja wao ni straika Elvis Rupia aliyeikacha ligi ya KPL Juni 2018 baada ya mzunguko wa kwanza wa msimu huo akiwa anaichezea Nzoia Sugar na kujiunga na Power Dynamos ya Zambia.

Wakati akiondoka, Rupia alikuwa akiongoza jedwali la ufungaji magoli akipachika mabao 15. Hata hivyo, baada ya maisha kuwa magumu Power Dynamo alikoshindwa kung’aa alirejea nchini na kusajiliwa na Wazito FC.

Ni mmoja wa wazito wanaotegemewa kuisaidia timu hiyo kuipokonya Gor ubingwa wao naye kaahidi kufanya hivyo.

“Maisha kule yalikuwa magumu, nilishindwa kabisa kuingiliana na mazingira ya kule. Halafu katika ligi ya kule soka wanalocheza ni la kimabavu na la kasi ya ajabu. Nilipambana sana na angalau nilihusika kwenye mechi 20,” Rupia alifafanua.

Na sasa anasema uzoefu alioupata huko ndio kauleta KPL na hivyo wapinzani wa Wazito FC wawe tayari kuhisi uzito.

“Nipo kwenye shepu nzuri na nafurahia kurejea KPL. Ninachosubiri tu ni msimu uanze. Lengo langu ni kupachika magoli 15 kwenye mzunguko wa kwanza kisha niongeze kadhaa mzunguko wa pili,” Rupia katahadharisha.

Lakini si yeye tu anayeapa kuchachisha tu, yupo pia mzito mwingine mwenye uzoefu wa KPL aliyesajiliwa, Karim Nizigiyamana. Beki huyo wa kulia aliwahi kuichezea Gor kabla ya kurejea katika ligi ya kwao.

Licha ya kuwa na umri wa miaka 30, Wazito waliamua kumsajili Mburundi huyo kutokana na tajriba na uzoefu wake wa KPL.

Nizigiyamana kaahidi kuwakomoa wakosoaji wake wanaohoji kuwa ni mzee sana kuzalisha matokeo kama alivyokuwa akifanya alipokuwa na Gor hasa zile krosi zake hatari na kasi ya ajabu.

“Nimekuja kuwafanyia kazi kwa roho moja na kujitolea. Watu wananiambia kama nitaweza sababu umri wangu umekwenda nami nataka wajue wamenichokoza ndio sasa watarajie kuona ubora wangu hata zaidi, tutasumbua sana,” Nizigiyamana kasema.

Nyota wengine waliosajiliwa katika kikosi hicho cha Wazito ni kiungo fundi Ali Bondo zamani akiichezea Gor, beki wa kushoto Abouba Sibomana, Derrick Otanga, Kevin Omondi na Joshua Otieno.